METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 27, 2018

DKT TIZEBA AFANIKISHA UPATIKANAJI WA MIL 63 KWA AJILI YA SHULE YA SEKONDARI BULUBA

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye Jubilee ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Buluba iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga juzi tarehe 25 Octoba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, WK)
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili eneo la shule ya sekondari Buluba kwa ajili ya kushiriki Jubilee ya miaka 50 ya shule hiyo iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga, juzi tarehe 25 Octoba 2018.
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye Jubilee ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Buluba iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga juzi tarehe 25 Octoba 2018.

Na Mathias Canal, WK-Shinyanga

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) amefanikisha upatikanaji wa kiasi cha shilingi Milioni 63,975,800 kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu mbalimbali ya shule ya sekondari Buluba iliyopo Shinyanga Mjini inayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU).

Kiasi hicho cha fedha kimepatikana wakati wa harambee aliyoiendesha tarehe 25 Octoba 2018 wakati wa Jubilee ya miaka 50 ya shule hiyo ambapo awali ilitanguliwa na mahafali ya 48.

Katika harambee hiyo fedha taslimu kiasi cha shilingi Mil 17,448,000 zilipatikana, Ahadi zilizotolewa ni Mil 20,365,800 huku vifaa vilivyochangwa ni Nondo moja pamoja na mifuko 1307 ya saruji vyenye jumla ya shilingi Mil 26,162,800 

Fedha hizo pamoja na vifaa vya ujenzi vitatumika kutatua changamoto za shule hiyo ambazo ni pamoja na kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, Upungufu wa vitabu vya kujifunzia darasani, uhaba wa vyoo, sambamba na ujenzi wa uzio.

Vilevile utatuzi wa changamoto ya vifaa vya ufundishaji kama kompyuta, kuboresha maktaba pamoja na upatikanaji wa vitabu vya kutosha.

Awali, akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza katika hafka hiyo ya Jubilee ya miaka 50, Waziri Tizeba alimuagiza Mrajisi wa vyama vya Ushirika Ndg Tito Haule kufuatilia taarifa za mapato na matumizi ya shule hiyo haraka iwezekanavyo.

" Wakati tunachangia fedha hizi kwa ajili ya shule na mimi kwa dhamana niliyonayo ninamuagiza Mrajisi wa vyama vya ushirika aje apate ripoti ya fedha ya hii shule kwa sababu hii shule ni mali ya umma" Alisisitiza Dkt Tizeba

Alisema kuwa serikali imechoka kusikia Ushirika ni sawa na wizi hivyo imeweka juhudi za makusudi za kuwabaini wabadhilifu wa mali za Ushirika na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

"Tunataka tusikie Ushirika ni sawa sawa na Maendeleo ya wakulima au wana Ushirika wenyewe" Alisema

Katika Jubilee hiyo ya Shule ya sekondari Buluba iliyoanzishwa mwaka 1967, Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb).

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com