METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 27, 2018

MJUMBE BARAZA KUU UVCCM TAIFA NDG OMEGA THOBIAS AWAASA WAHITIMU KUJIONGEZA KWA KUTAFUTA UJUZI





Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM TAIFA (Njombe) ambaye pia ni Afisa kutoka UVCCM Makao Makuu Ndugu Omega Thobias amekuwa Mgeni Rasmi kwenye mahafali ya Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Migombani iliyopo Tabata Segerea Jijini Dar Es Salaam. 

Ndg Omega Thobias akiiwakilisha UVCCM kupitia Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA Ndg Hassan Bomboko amewaasa wanafunzi wanaohitimu kuwa raia wema pindi watakapomaliza mitihani yao na ili kuondokana na vitendo viovu mitaani amewaomba Wazazi, Walezi, Ndugu, Jamaa na marafiki wa wanafunzi kuendelea kuwasimamia kwa kuwaendeleza kielimu hasa kuwapeleka Vyuo vya VETA ili wapate Ujuzi utakao wasaidia maishani mwao. 

"Ujana wetu tusiutumie vibaya kwa kujiona sisi ndio wasomi kuliko wengine, Tuweni wanyenyekevu na wenye uchaji wa kujifunza mambo mbalimbali yenye tija ili tuweze kuisaidia serikali yetu inayoongozwa na Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli inayotekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi wa mwaka 2015/2020 hasa katika sera ya Tanzania ya Viwanda" amesema Ndg Omega Thobias.

Ndg Thobias amewajuza wanafunzi hao umuhimu wa kuwa na ujuzi na kusema kwamba Ujuzi haufi wala kupotea, hivyo msiishie kusoma tu darasani ili mfaulu mitihani ni vema kila akaona kitu akipendacho na anachokimudu akaendelea kujifunza kwa muda wake wa ziada iwe ni kusuka nywele, ushonaji, uhunzi, ufundi umeme, upambaji, uchoraji, na sanaa yote kwa ujumla. 

Awali, Mgeni Rasmi alipata nafasi ya kuonyeshwa Majaribio ya Kisayansi (*Experiments) kwenye *Maabara Shuleni hapo ambapo wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaohitimu na wale wa Kidato cha tatu na cha kwanza walifanya vizuri kwa vitendo. 

Aidha, Wanafunzi wa Sekondari ya Migombani walionyesha uwezo wao kupitia vipaji kwa uigizaji, ushairi, muziki wa kizazi kipya, ngoma na uigaji sauti ambapo Mgeni Rasmi aliwasisitiza kuvithamini vipawa walivyonavyo na kuviendeleza ili kuja kunufaika navyo kwani Kipaji ni Mtaji. 

Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Migombani Mwl Mama Chalamila ameusifu Utendaji wa Rais Dkt Magufuli na Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako na Uongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kwa jinsi ulivyo karibu na Taasisi za kiraia na  kiserikali na kwa kipekee UVCCM kukubali mwaliko wao kwenye mahafali hiyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com