WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya
Maliasili na Utalii kukamilisha zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika maeneo
yote ya hifadhi ifikapo Desemba 30, 2017.
Agizo hilo limekuja baada ya kuwepo kwa migogoro ya
mipaka kati ya wananchi na hifadhi ambapo baadhi ya wananchi wanaendesha shughuli
za kijamii ndani ya hifadhi.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Novemba 16, 2017)
wakati akijibu swali la mbunge wa Ulyankulu, Bw. John Kadutu wakati wa kipindi
cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma.
Bw. Kadutu alitaka kujua hatua zilizofikiwa na
Serikali katika uwekaji wa alama za mipaka katika maeneo mbalimbali ya hifadhi
ili kuwaondolea wananchi usumbufu.
“Wizara ifanye mapitio ya maeneo yote ya hifadhi
ambayo bado hayajawekewa alama za mipaka na kukamilisha zoezi hilo ifikapo tarehe
30, Desemba, 2017.”
Pia Waziri Mkuu amewataka wananchi wote wanaoishi
maeneo ya karibu na hifadhi hizo au hata ndani watoe ushirikiano kwa wataalamu
ili kuweza kukamilisha zoezi hilo kwa wakati.
Waziri Mkuu amesema wananchi wanaoshi katika maeneo
yaliyoko ndani ya hifhadhi wawaache wataalamu wakamilishe zoezi hilo na baada
ya kukamisha Serikali itafanya mapitio na kisha kutoa maamuzi kwa manufaa ya
Taifa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema sheria namba moja ya Ajira za Wageni ya mwaka 2015 inaruhusu utoaji wa
vibali vya ajira kwa wageni kwa muda wa miaka miwili. “Hata hivyo vinaweza kuongezwa kulingana na mahitaji
hadi kufikia vipindi viwili.”
Hata hivyo, Serikali imewapa
masharti wageni wanaoomba vibali vya kufanya kazi nchini kuandaa mpango wa
kuwarithisha ujuzi Watanzania ili kuchukua nafasi za wageni hao mara baada ya
muda wa vibali vyao kumalizika.
Pia Serikali inayataka makampuni yote uwekezaji kutoa kipaumbele cha
ajira kwa Watanzania kwa kuwa kwa sasa tunao Wataalamu wa kutosha katika fani
mbalimbal
Waziri Mkuu ameyasema hayo
wakati akijibu swali la Mbunge wa Kuteuliwa Bw. Abdallah Bulembo aliyetaka
kufahamu wageni wanaokuja kufanya kazi nchini wanaruhusiwa kufanya kazi kwa
muda gani.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P.
980,
DODOMA.
ALHAMISI, NOVEMBA 16, 2017.
0 comments:
Post a Comment