WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka
Wizara ya Kilimo ifanye utafiti wa kina ili kupata aina bora ya mbegu za pamba
zitakazowanufaisha wakulima.
Amesema ni lazima utafiti
huo ufanyike kwa kuzingatia aina ya udongo unaopatikana katika kila mkoa
unaolima pamba.
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Jumanne, Novemba 14, 2017) alipozungumza na wabunge wanaotoka katika mikoa
inayolima pamba, Bungeni mjini Dodoma.
“Mbegu za pamba ziko nyingi
na zina migogoro. Mbegu nyingine zina manyoya, nyingine zina vipara hivyo
lazima utafiti wa kina ufanyike ili kupata aina bora.”
Alisema Wizara ya Kilimo itumie
taasisi zake vikiwemo vyuo kufanya uchunguzi na kubaini ni aina gani za mbegu
zinafaa kutumika kulingana na eneo husika.
Alisema utafiti huo ambao
utabainisha aina ya mbegu inayofaa kulingana na aina ya udongo katika kila eneo
ili kumuwezesha mkulima kupata mazao ya kutosha.
Pia aliwataka Maofisa Kilimo
katika mikoa inayolima mazao makuu ya biashara waweke kipaumbele katika
kuyasimia mazao hayo.
Waziri Mkuu alisema Maofisa
hao lazima wahakikishe wanayasimamia vizuri mazao hayo ambayo ni korosho, chai,
pamba, kahawa na tumbaku ili yawe na tija.
Alisema Serikali imeweka
mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza
kupungua likiwemo na zao la pamba.
Waziri Mkuu alisema Serikali
inataka kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la pamba kuanzia hatua za
maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.
“Tunataka kulifanya zao hilo
ambalo lilikuwa likijulikana kama dhahabu nyeupe lifikie kiwango cha juu cha
uzalishaji, hivyo kuongeza tija kwa wakulima.”
Pia Waziri Mkuu aliwaagiza
Maofisa Kilimo katika mikoa hiyo wafanye sensa ili kutambua idadi ya wakulima
wa pamba na ukubwa wa mashamba yao.
Alisema lengo la sensa hiyo
ni kutambua idadi ya wakulima na ukubwa wa mashamba yao ili kurahisisha
usambazaji wa pembejeo kulingana na mahitaji.
Wakizungumza katika
mkutano huo baadhi ya wabunge waliiomba Serikali kuhakikisha zao hilo
linaboreshwa ikiwa ni pamoja na kuwafikishia wakulima pembejeo kwa wakati.
Kwa upande wake Mbunge
wa Itilima Bw. Njalu Silanga aliiomba Serikali izibane Halmashauri ili kuhakikisha
fedha za miradi ya kilimo zinatumika ipasavyo.
Bw. Silanga alisema
msukumo wa Serikali wa kufufua zao la pamba umeanza kuzaa matunda, hivyo
aliiomba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutafuta masoko ya kutosha.
Naye Mbunge wa Tarime
Mjini, Bi Ester Matiko ameiomba Serikali kuwaelimisha wananchi na kuwahamasisha
kulima kilimo hicho ili waachane na kilimo cha bangi.
“Serikali ikitilia
mkazo katika usimamizi wa mazao hayo tutasonga mbele na Tanzania ya viwanda
tutaiona. Wakulima waelimishwe kuwa mazao hayo yana tija, hivyo wataachana na
kilimo cha bangi.”
Bi. Ester alisema kati
ya mazao makuu matano ya biashara manne yanalimwa katika jimbo lake ambayo ni
chai, pamba, kahawa na tumbaku, hivyo wakulima wakipewa elimu ya kutosha juu za
mazao hayo watapata tija.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P.
980,
DODOMA.
JUMATANO, NOVEMBA 15, 2017.
0 comments:
Post a Comment