Na Mwandishi Maalum
Abbas Kondo Gede na Albeto Mandes
wamehukumiwa kwenda jela miaka 22 kila moja kwa kosa la kujihusisha
na usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya Cocaine na Heroin.
Washitakiwa hao ambao walitenda makosa
yao kwa nyakati tofauti wamehukumiwa pia kulipa faini ya jumla ya
shilingi 320.7 milioni.
Hukumu ya Abbas Kondo Gede ya kwenda
jela miaka 22 na kulipa faini ya jumla ya shilingi 175,764,000/=
imetolewa leo ( Jumatano) na Mhe. Jaji Korosso baada ya
kujiridhisha pasipo shaka kwamba, mshtakiwa alikuwa na hatia ya
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Abbas Kondo Gede mtanzania, na mkazi
wa mtaa wa Lindi, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, na ambaye
alikuwa ni mcheza mpira wa miguu. Alikamatwa tarehe 14/5/2011 katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
akitokea Sao Paulo, Brazil, kwa usafiri wa Shirika la Ndege la
Quater akiwa na kete 77 sawa na gramu 1,171.75 za cocaine
zilizokuwa na thamani ya shilingi 58,588.000/= milioni.
Kesi ya Abbas Gede iliendeshwa na
Mawakili wa Serikali Batilda Mushi na Frank Tawala ambapo katika
maelezo yao waliiomba Mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa
wengine wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Kwa upande wa Albeto Mendes ambaye ni
raia wa Guinea Besau yeye alikamatwa tarehe 15/4/2012 katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa na
gram 1,277.41 za Heroine zilizokuwa na thamani ya shilingi milioni
57,483.000/= akiwa katika harakati za kusafiri kwenda nchini Mali.
Hukumu ya Albeto Mendes ya kwenda
jela miaka 22 na kulipa faini ya shilingi 144,955,700/= imetolewa leo
( jumatano) na Mhe. Jaji Mfawidhi Matogolo baada ya kujiridhisha
pasipo shaka kwamba mshtakiwa alikuwa na hatia.
Mawakili wa Serikali walioendesha kesi
hiyo na kuiomba Mahakama kutoa adhabu kali walikuwa ni Joseph
Maugo ambaye ni Wakili wa Serikali Mwandamizi na Wakili Clara
Chalwe.
Imetolewa na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Dar es Salaam
20/9/2017
0 comments:
Post a Comment