Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Shinyanga
Mheshimiwa Azza Hilal (CCM) amewataka akina mama kujitahidi kuwekeza
katika elimu kwa watoto hususani watoto wa kike na kuwa mstari wa mbele
kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora.
Mheshimiwa Azza Hilal (pichani)
ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 20,2017 katika ukumbi wa Mountain
View Hotel uliopo katika kata Tinde wilaya ya Shinyanga wakati akifungua
Mafunzo ya ujasiriamali,fedha na mikopo kwa akina mama yaliyoandaliwa
na Benki ya CRDB tawi la Shinyanga.
Mbali na kuwaasa akina mama kutumia
vyema mikopo wanayopata kuitumia kwa malengo waliyokusudia,pia
aliwakumbusha kuwekeza kwa watoto wao.
Alisema mkoa wa Shinyanga ni miongoni
mwa mikoa inayoongoza nchini kwa kuwa na takwimu kubwa (asilimia 59) ya
mimba za utotoni na ndoa za utotoni hivyo jitihada mbalimbali za pamoja
zinahitajika ili kuondoa vitendo hivyo ambavyo vinawanyika haki watoto
wa kike kuendelea na masomo yao.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha kuwa
sisi akina mama kuwa tuna wajibu mkubwa kuhakikisha watoto wetu wa kike
wanapata elimu iliyo bora,kuhakikisha pia watoto ambao hawakupata fursa
ya kufaulu mtihani wa darasa la saba ili kuendelea na masomo ya kidato
cha kwanza tunawatafutia njia mbadala ya kuweza kujikomboa na maisha
badala ya kukimbilia kuwaozesha”,alieleza Hilal.
“Kumekuwa na tabia, mtoto akiingia
darasa la saba anaambiwa na wazazi wake kuwa akafanye vibaya kwenye
mtihani,naomba tuanze sisi akina mama kukataa,kwanini unakubali mtoto
wako aambiwe na baba yake kuwa akafeli mtihani?”,alihoji mbunge huyo.
Aidha alisema ili kuondoka kwenye
takwimu za kuitwa watu ambao hawajasoma ni vyema akina mama wakawa
mstari wa mbele katika kupigania haki za watoto.
“Wenye kulibeba hili ni akina mama kwa
sababu akina baba tunajua wametanguliza pesa mbele,najua hakuna ambacho
mwanamke anaweza akaamua kukifanya na kikashindikana,naomba tuanze
kuwapatia watoto malezi ya kupenda elimu na kuepuka vishawishi wakiwa
wadogo”,alisema Hilal.
“Niwaombe sana tuwe karibu na watoto
wetu wa kike, ili waweze kukushirikisha kwa jambo lolote watakalokutana
nalo,usipokuwa karibu na mtoto wako,hata kama atabakwa hawezi kujibu
kwako,lakini kama umejenga utamaduni wa kuongea naye kama rafiki
yako,kama ndugu yako wa karibu hawezi kusita kukwambia jambo lolote zuri
ama baya litakalokuwa limemtokea”,alieleza Mhe. Hilal.
Mbunge huyo pia alieleza kusikitishwa na
vitendo vya baadhi ya wazazi kuficha matukio ya watoto wanapofanyiwa
vitendo vya kikatili kwa watoto wa kike.
“Watoto wengi wa kike wanafanyiwa
vitendo vya kikatili ikiwemo kubakwa,kwa taarifa nilizopewa polisi
wazazi mnaficha vitendo vya kikatili dhidi ya watoto,kwanini mnaficha
vitendo hivi viovu? Mtoto anafanyiwa vitendo vibaya halafu mzazi
unaficha?,inakusaidia nini?,ni bora ukakubali fedheha ya siku moja
lakini haki ya mtoto wako ikapatikana”,alisema.
“Inasikitisha sana pale mnapoitwa kutoa
ushahidi wa kesi za ukatili dhidi ya watoto halafu mnakataa,kwa kweli
hamuwatendei haki watoto wetu,Kama mzazi unatetea uovu wa namna hii wewe
ni muuaji kwa sababu wewe mzazi usipotoa ushirikiano hatma ya kesi
haitakuwepo matokeo yake mtabaki kulalamika tu kuwa watuhumiwa
mnawapeleka polisi lakini mnawaona wapo tu mtaani,sasa mtuhumiwa
ataachaje kuwepo wakati hutoi ushirikiano?”,aliongeza Mhe. Hilal.
Aidha aliwataka wadua wote wa haki za
watoto kuendelea kulaani vitendo vya ukatili dhidi ya watoto huku
akiwasisitiza wazazi na walezi watoto kutofumbia macho vitendo na
kumaliza kesi kienyeji kwani haki za watoto zinapotea.
Katika hatua nyingine kutokana na
maendeleo katika sayansi na teknolojia aliwatahadhalisha wazazi na
walezi kuwa makini na matumizi ya mitandao kwani baadhi ya watoto
hususani wanaosoma katika shule zenye mabweni ‘Boarding’ wanafanya
michezo mibaya kutokana na mambo wanayoyaona mitandaoni.
Mbunge huyo aliishukuru Benki ya CRDB
kkutoa elimu kuhusu masuala ya fedha na mikopo elimu ambayo itawasaidia
wananchi kuendesha biashara zao vizuri.
Hata hivyo Meneja wa Benki ya CRDB
alisema benki hiyo itaendelea kufungua matawi katika maeneo mbalimbali
ya vijijini na kuwapatia elimu wajasiriamali waliopo kwenye vikundi
mbalimbali.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
0 comments:
Post a Comment