Shirika
la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Mitaji na Maendeleo (The United Nations
Capital Development Fund-UNCDF), ikishirikiana na kampuni ya Ensol
Tanzania Ltd. (Ensol) wamezindua mfumo wa umeme wa nishati ya jua katika
kijiji cha Mpale kilichopo wilaya ya Korogwe, na hivyo kuwezesha umeme
katika eneo hilo kwa mara ya kwanza.
Mradi
huo ulizinduliwa rasmi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini
Dk. Juliana Pallangyo ambaye aliipongeza kampuni ya Ensol na washirika
wake ikiwemo UNCDF kwa juhudi zake kubwa za ushawishi wa umeme hasa
umeme mbadala wa jua ili kuboresha ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa
mtu binafsi na taifa.
Dk. Pallangyo alisema kwamba serikali ya Tanzania inawashukuru watu wa Ensol kwa juhudi zao kubwa za kupeleka umeme vijijini.
Alisema
kwa Ensol kuweza kufikisha umeme katika maeneo ya ndani kabisa ya
kijiji cha Mpale, kuwaunganisha wananchi na umeme wa saa 24 na
wamefanikiwa kubadili maisha ya wananchi hao.
Alitoa wito kwa jumuiya hiyo kutumia umeme sio kwa kuwasha taa pekee bali pia katika kusukuma mbele kazi za uzalishaji.
Dk.
Pallangyo alifurahishwa na kituo cha afya Mpale kuunganishwa na mfumo wa
nishati ya jua na kuwataka maofisa wa wilaya kulipa Ankara zao kwa
wakati ili kuhakikisha kwamba huduma zinapatikana bila kukoma kwa
wananchi.
Kijiji
cha Mpale kipo katika maeneo ya milimani katika kata ya Mpale wilaya ya
Korogwe mkoani Tanga. Kijiji chenye wakazi 9000 na nyumba 730, tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1972 hakijawahi kuwa na umeme.
Wengi
wa wanavijiji walikuwa wakitegemea mno mafuta ya taa ambayo kwa kiasi
kikubwa yalikuwa si masafi kwa ajili ya kuwashia taa zao.
Mpaka
sasa Ensol imeshaunganisha umeme kwa kaya 50. Aidha mpango unafanyika
wa kutanua mradi ili ifikapo Juni 2018 nyumbna 250 ziwe zimeunganishwa.
Mreadi
huo wa kuunganisha wanakijiji na nishati inayozalishwa kwa nguvu za jua
ulianza mwaka 2014 wakati Ensol walipozuru vijiji kadhaa vya mkoa wa
Tanga kuangalia uwezekano wa kupata kijiji cha mfano na kubaini kuwapo
kwa kijiji cha Mpale.
“Ushirikiano
wa UNCDF ulikuwa muhimu katika mradi huu gridi ndogo ya nishati ya jua.
Pamoja na kwamba tulipokea fedha kutoka UNCDF na wadau wengine, UNCDF
imekuwa ndio chombo cha kuingiza masuala ya kitaalamu na ushauri
mwingine. Kushirikiana na UNCDF kumeongeza kuaminika miongoni mwa wadau
na taasisi za kifedha,” anasema Prosper Magali, Meneja wa mradi wa Mpale.
Bw. Magali aliongeza,
“Ninaamini kama si msaada wa UNCDF huu mradi usingekuwepo hapa ulipo.
Tumepokea fedha kutoka EEP na wafadhili wengine. Lakini ni kwa sababu ya
UNCDF tumeweza kupata fedha kutoka katika taasisi nyingine za
ufadhili”.
Mkuu
wa UNCDF Tanzania, Peter Malika alisema kwamba umeme ni chanzo cha
maendeleo na kwamba sekta binafsi ina nafasi ya kusaidia serikali katika
juhudi zake za kuangaza maeneo ya vijijini.
“Kwa
kuwezesha Mpale kuwa na umeme tunawasaidia wananchi wa kijiji hiki
kufanya maendeleo ya kiuchumi. Fursa nyingi za kiuchumi zitaibuka, kituo
cha afya kitaweza kuboresha huduma zake na wanafunzi watakuwa na muda
zaidi wa kusoma.”
Mafanikio
ya mradi huo ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya serikali ya
mitaa na wananchi wakati wote wa mchakato wa kufanikisha mradi.
“Wananchi
wamefarijika tangu kampuni ya Ensol itembelee kijiji hicho kwa mara ya
kwanza na kuzungumza kuhusu uletaji wa umeme wa nishati ya jua. Tumekuwa
na ushirikiano mkubwa tangu siku ya kwanza ambapo wamekuwa
wakitushirikisha,” anasema Mwenyekiti wa kijiji Augustine Rugambwa.
Bw.Rugambwa aliongeza:
“Nimefurahishwa sana kwamba mradi huu umekuja wakati wa uongozi wangu.
Ni nafasi adimu ambayo nitaikumbuka maisha yangu yote. Tunawashukuru
sana UNCDF kwa kutukumbuka hata sisi tuliopembezoni. Kupitia Ensol
tutaingiza nishati ya umeme majumbani mwetu. UNCDF tunawashukuru kwa
msaada wenu huu. Kamwe hatutawasahau.”
“Tunaamini
kwa msaada tulioupata kutoka UNCDF na wengine, mradi huu utakuwa
endelevu na utakaokuwa unatengeneza faida kwani wateja watakuwa wanalipa
Ankara zao kila mwezi. Kwa hiyo fedha zitakazopatikana zitatumika
kuufanya mradi kuwa endelevu,” alisema Prosper.
“Tunatumia
mradi kama huu kama mafunzo. Lengo letu ni kuwa na miradi mingine kama
hii 15 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Tumetembelea maeneo ya
nyanda za juu Kusini kuona vijiji vinavyoweza kupatiwa mradi wa umeme wa
jua. Tumekubaliana na serikali za mikoa na tawala za mitaa kuwapeleka
nishati ya umeme jua na tunatarajia kuwaunganisha na watu nyumba elfu
kumi.
Kuna vijiji vingi kama hiki cha Mpale vinavyohitaji umeme, kwa
hiyo fursa za umemejua ni kubwa sana!” aliongeza Prosper.
Bw
Malika alisema kwamba UNCDF itaendelea kufanyakazi kwa karibu na Ensol
na taasisi nyingine za umma na binafsi kuwezesha kufikisha umeme katika
maeneo yanayofikika wka shida nchini Tanzania.
0 comments:
Post a Comment