Katika kutekeleza kwa vitendo sheria ya
Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa mifugo ya mwaka 2010 sambamba na kanuni zake za mwaka 2011, halmashauri ya wilaya ya Tunduru imefanya uzinduzi wa upigaji chapa ng’ombe mapema wiki hii katika Kijiji cha Muhuwesi, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera.
Akisoma taarifa ya uzinduzi wa zoezi la upigaji chapa ng’ombe, Afisa Mifugo na Uvuvi wilaya Dk. Frank Mkoma alisema wilaya ya Tunduru ina jumla ya ng’ombe 62,685, mbuzi 5,974, kondoo 3,388 na nguruwe 2,650. Kati ya vijiji 157 vya wilaya ya tunduru ni vijiji 41 vilivyokwisha kufanyiwa matumizi bora ya ardhi na jumla ya hekta 11,480 zimetengwa kwa ajili ya malisho, eneo hili lina uwezo wa kulisha mifugo 11,480.
Dk. Mkoma alisema halmashauri kwa awamu ya kwanza wanatarajia kupiga chapa ng’ombe wapatao 62,685 na watapigwa chapa kwenye mguu wa nyuma upande wa kulia.
“Katika zoezi hili la upigaji chapa ng’ombe, wafugaji wote wa ngombe waliopo kwenye wilaya kuanzia mwenye ng’ombe mmoja hadi makundi makubwa watahusika, na maeneo yenye mifugo mingi ni yale yaliyopo pembezoni hasa katika kata ya Ngapa, Mkowela, Twendembele Na Misechela.”alisema Dk Mkoma.
Aliendelea kusema kuwa kupiga chapa ng’ombe kuna faida hasa katika suala zima la ufuatiliaji, usajili na utambuzi wa mifugo kwani huzuia wizi wa mifugo na uhamishaji wa mifugo usiofuata taratibu za kisheria hasa kwa wafugaji wenye makundi makubwa ambao uhama toka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta malisho bila kuwa na vibali vya kusafirishia mifugo.
“utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo huzuia wizi wa mifugo kwani utaratibu huu huhusisha utambuzi, usajili na ukusanyaji wa takwimu mbalimbali za mnyama kwa kipindi chote cha uhai wake ili kuwezesha ufuatiliaji, na pia kwa sasa sheria ya mifugo hairuhusu mnyama kuchinjwa au kuuzwa katika mnada bila kuwa na alama ya utambuzi”alisema afisa mifugo wilaya.
Kwa upande wa wafugaji walioshiriki katika zoezi la upigaji chapa ng’ombe walishukuru serikali kwa kutambua umuhimu wa kufanya utambuzi wa ng'ombe na pia wanaiomba serikali kuwatengea maeneo yenye malisho ya kutosha na kuwajengea miundombinu ili waweze kufuga kisasa.
“sisi tuko tayari kuhamia katika maeneo ambayo serikali imepanga kutupeleka ili kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa sababu sasa hivi tunalisha katika mashamba ya wakulima na wakati mwingine tunaingia katika hifadhi hivyo tunagombana na maliasili na wakulima kutokana na mazao yao kuliwa na mifugo yetu”alisema Mfugaji Songambele Lereshi.
Naye mfugaji Nyengela Msafiri alisema kuwa wanaenda kulisha katika mashamba ya wakulima na katika hifadhi za taifa na misitu ya jamii kutokana na maeneo waliyotengewa hayatoshelezi kwa malisho ya mifugo yao kutokana na nyasi kukauka hasa kipindi cha kiangazi.
“tumeipokea hii taarifa ya kupiga chapa ng’ombe kwa furaha kubwa sana sisi wafugaji kwa sababu itaendea kuondoa kabisa wizi wa mifugo yetu na pia kutambuliwa na serikali na kupewa maeneo ya kufugia, ila wito wangu kwa serikali ni kuomba watutengee maeneo yenye malisho na maji ya kutosha nasi tutaacha kuhamahama” alisema Mandi Karwa.
Naye Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa zoezi la kupiga chapa ng’ombe alisema zoezi hili ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2015/20 ya kupunguza migogoro kati ya wakulima nawafugaji, na pia kufanya ufugaji wa kisasa.
Aidha Dc Homera aliendelea kusema kuwa serikali imekuwa ikishirikiana na shirika la dini la Anglikana chini ya mradi wa AMCC ambao wanatekeleza mradi katika wilaya ya tunduru na wanaprogramu ya kopa ng’ombe lipa ng’ombe ambao wanatoa mifugo ya mbuzi na ng’ombe kwa wananchi.
“kwa mwaka 2016 AMCC kupitia mradi wa CHIP walitoa ngombe 45 na mbuzi 60 na kwa mwaka huu 2017 wanatarajia kutoa ng’ombe 100 na mbuzi 120”.
Aliendelea kusema kuwa maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya kupeleka mifugo hasa kwa wafugaji wenye makundi makubwa ya ng’ombe ni Mkowela, Ngapa na Liwangula na wafugaji ambao mifugo yao itapigwa chapa ndio ambao wataanza kuelekezwa kuelekea huko.
Mhe. Homera alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wake wainaishi kwa Amani na Utulivu na kuongeza mapato yatokanayo na mazao ya mifugo kwani wafugaji wakifuga vizuri wanaweza kuzalisha bidhaa nyingi zinazotokana na mifugo ikiwa bidhaa za biashara pamoja na chakula.
Mkuu wa wilaya aliomba ushirikiano toka kwa wafugaji ili wananchi waweze kuishi kwa Amani na pia aliwataka wafugaji kufuata sheria, kanuni na taratibu za vijiji husika wanapoishi ili kuondoa migogoro kati ya mkulima na mfugaji wakati serikali ikiendelea na mipango ya kuwatengea maeneo na kuboresha miundombinu.
Aliendelea kusema kuwa anawashukuru wafugaji na wananchi wote waliopokea zoezi la upigaji chapa ng’ombe kwa vitendo kwani zoezi hili ni muhimu sana na lengo la serikali sio kuwaibia au kutaifisha mifugo yenu kama baadhi ya watu wanavyodanya na kupotosha.
“Nia ya serikali ni kurahisisha ufuatiliaji, usajili na ukusanyaji wa takwimu halisi za mifugo katika wilaya yetu na Hakuna mfugaji yeyote ambaye mifugo yake itachukuliwa kwani serikali haina nia ovu kwa wananchi wake.”alisema Mkuu wa wilaya.
Alitoa rai kwa wafugaji ambao hawajajitokeza katika zoezi la kupiga chapa wafanye hivyo kwani wilaya ya Tunduru haipo tayari kuendelea kuishi nao na kama watagoma mpaka zoezi litakapokamilika tarehe 26/10/2017 basi waondoke katika maeneo ya Tunduru.
Hata hivyo Mhe. Juma Homera alimazia kwa kutoa rai kwa wafugaji wote wanaochungia katika hifadhi za taifa,misitu ya hifadhi ya jamii na mapori tengefu kuondoa mifugo yao kwani serikali haitamfumbia macho mfugaji yeyote au mkilima anayefanya shughuli za kibinadamu katika mazingira hayo.
0 comments:
Post a Comment