Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akibofya kitufe kuashiria
uzinduzi rasmi wa Muonekano Mpya wa Gazeti la Michezo la Mwanaspoti
Jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia tukio hilo ni baadhi ya Viongozi
waandamizi wa Kampuni ya Uchapishaji Magazeti ya Mwananchi
Communications Ltd (MCL).
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na baadhi ya Viongozi
waandamizi wa Kampuni ya Uchapishaji Magazeti ya Mwananchi
Communications Ltd (MCL) wakishangilia mara baada ya uzinduzi wa
Muonekano Mpya wa Gazeti la Michezo la Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akichomoa gazeti jipya la
Michezoa la Mwanaspoti ambalo lina muonekano mpya wa kisasa zaidi mara
baada ya kulizindua Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya Uchapishaji Magazeti ya Mwananchi Communications Ltd
(MCL), Bw. Francis Nanai (kulia) wakiwaonyesha Waandishi wa habari
muonekano mpya wa gazeti la michezo la Mwanaspoti mara baada ya uzinduzi
Jijini Dar es Salaam.
Na Benedict Liwenga-WHUSM.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameipongeza Kampuni ya
Uchapishaji Magazeti ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa
jitihada kubwa wanazozifanya katika kusimamia maadili kwa kuhabarisha na
kuielimisha jamii ya Kitanzania.
Pongezi hizo amezitoa jana wakati
wa Uzinduzi wa Muonekano Mpya wa gazeti pendwa la michezo la Mwanaspoti
linalochapishwa na Kampuni hiyo.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa, mara
kwa mara MCL imekuwa ikiisaidia jamii kwa kujihusisha katika masuala
mbalimbali ya kijamii kama vile wakati wa tetemeko la ardhi Mkoani
Kagera imeweza kutoa mchango wake mkubwa kwa jamii na daima imekuwa
ikilinda maadili na weledi wa kazi ya uandishi kwa wafanyakazi wake
jambo ambalo linaonyesha ushirikiano mzuri baina ya Serikali, Kampuni na
jamii.
“Mimi nawapongeza na kuwashukuru
sana MCL kwakuwa mstari wa mbele katika kulinda maadili katika kazi
zenu, endeleeni kulinda maadili kwa kuhabarisha na kuielimisha jamii,
sijaona mkivunja maadili ya kazi zenu na hakika mnajijengea sifa nzuri
kwa wengine”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa, kwa sasa kumeibuka
wimbi kubwa la Waandishi wa habari (Makanjanja) ambao hawana vyeti wala
weledi wa kufanya kazi ya uandishi wa habari na hao wamekuwa kila
wakati wakirusha taarifa zisizo sahihi hususani katika mitandao ya
kijamii jambo ambalo Serikali haiwezi kulifumbia macho.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa MCL, Bw. Francis Nanai amesema kwamba lengo la kampuni hiyo
kuja na muonekano mpya wa gazeti hilo ni kuwapa ladha mpya wasomaji wake
nchini kote, na hiyo ni mara ya sita kwa gazeti hilo kubadilishwa
muonekano wake tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001.
“Sisi kama wadau wa michezo
tumewasikiliza wasomaji wa gazeti letu na tukayafanyia kazi mawazo yao
na ndiyo maana tukaamua kuja na muonekano mpya wa gazeti hili ambao uko
kimataifa zaidi”, alisema Nanai.
Aliongeza kuwa, gazeti hilo
lilianzishwa na waandishi wa tatu mwaka 2001 na lilikuwa likitoa nakala
3,000 kwa siku ambapo kwa sasa kuja kwa muonekano mpya wa gazeti hilo
kutaongeza idadi ya wasomaji tofauti ilivyokuwa mwanzo na idadi ya
uchapishaji imeongezeka hadi kufikia nakala 60,000 kwa siku.
0 comments:
Post a Comment