METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 26, 2017

Halmashauri za wilaya zatakiwa kutenda haki

Na Mwandishi Wetu, Mwanza 

Watendaji, Wakuu wa Idara na Madiwani katika halmashauri ya manispaa ya wilaya ya Ilemela wametakiwa kutekeleza majukumu yao ya kiajira, kitaalam na uwakilishi wa wananchi katika chombo hicho mkoani hapa. 

Pia wameshauriwa waendelee kusimamia vyema na kwa umakini majukumu  yao ya  msingi katika azma  ya kuisaidia serikali hususan kukabiliana na vitendo vya ufisadi , ubadhirifu na wizi 

Rai hiyo imetolewa  na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM  Shaka Hamdu Shaka alipozungumza na madiwani, wakuu wa idara na watendaji katika Manispaa ya halmshauri ya wilaya ya Ilemela. 

Shaka alisema kazi ya uwakilishi, utendaji ni zile za kitaalam zote haziwezi kupata manufaa na matokeo chanya iwapo  dhana za uadilifu, uwajibikaji,  wazi, ushirikishwaji na umakini zitalegalega au kukosekana. 

Alisema ili maendeleo yaweze kupatikana katika halmshauri yoyote nchini kuna ulazima, haja na shuruti ya watendaji, madiwani na wataalam kufanya kazi kwa ukaribu, upendo, ushirikiano na uzalendo 

"Halmashauri za wilaya ziko karibu na maisha ya watu  kila siku na wakati wote, ndizo zinazojua wananchi wana kero zipi, madiwani kuweni  kiungo kati ya wananchi na halamshauri , watendaji tekelezeni na kusimamia sera kwa kushirikiana na wakuu wa idara "Alisema Shaka 

Alieleza kuwa kitendo cha ufujaji miradi ya maendeleo inayoanzishwa kwa fedha zinazoletwa na  serikali na washirika wa maendeleo zinahitaji kutunzwa na kutumika kwa umakini na kwa malengo husika. 

"Hatutaki kuona vichuguu vya mchwa kwenye halmashuri zetu nchini, wezi na wabadhirifu wa mali na miradi ya umma, wasionewe muhali, wafufukuzwe kazi na kufikishwe katika vyombo vya sheria mara moja"Alisema shaka 

Pia aliwataka madiwani wakatae kupitisha bajeti zisizo na maslahi kwa maendeleo ya halamshauri na wananchi ambazo hudumaza huduma za jamii na fedha za umma kupotea hovyo. 

Hata hivyo shaka alipongeza ushirikiano uliopo kati ya halmshauri ya minispaa wilaya Ilemela, ofisi ya Mkuu wa wilaya na Chama Cha Mapinduzi toka ngazi ya Mkoa,Wilaya na Jumuiya za ccm wakitambua wote wanadhima ya kuhakikisha ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020 inatekelezwa kwa mafanikio makubwa. 

Alisema bila ya kuwepo mahusiano mema, masikilizano ya kutosha,  ushirikiano, utendaji wa kazi za chama, Serikali na halmshauri, unaweza kukwama na malengo yake kuweza kuvia.

Naye Mkurugenzi wa halmshauri ya Manispaa wa Ilemela John Wanga  alisema halmashauri yake itaendelea kutii sheria za nchi, kufuata kanuni na taratibu husika hatimae yatokee matokeo ambayo yatawanufaisha wananchi na kuwaondolea kero sambamba na kuhakikisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi unasimamiwa vizuri. 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com