METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 16, 2019

HALMASHAURI KASULU KUPAMBANA NA MIMBA ZA UTOTONI


Na Emmanuel Michael Senny, Kigoma 

Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma, imeanza kuchukua hatua na kuweka mikakati ya kukabiliana na ongezeko la wasichana wanaojifungua katika umri mdogo na kulazimika kukatisha masomo hali ambayo inaathiri afya zao pamoja na watoto. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu Fatina Laay,  alibainisha hayo mwishoni mwa wiki iliyopita na kuongeza kuwa pamoja na utungwaji wa sheria ndogo katika halmashauri, walipanga kuongeza utoaji wa elimu katika ngazi ya familia.

Aidha alisema mkakati mwingine ni kuanza kutoa mikopo ya biashara ndogondogo kwa wasichana waliokatisha masomo baada ya kujifungua ili wajikwamue kiuchumi na kuweza kutunza familia huku akiwataka wasikate tamaa.

"Ukosefu wa elimu umewafanya wasichana wengi kupoteza muelekeo katika maisha yao baada ya kubeba ujauzito, hivyo basi tunaazimia kuwaelimisha namna ya kuisha na kulea watoto wao bila shida lakini pia tunawaelekeza namna ya kutumia mikopo tunayowapa katika biashara ili waweze kumudu maisha ya kila siku" alisisitiza Bi Laay.

Kwa upande wao wasichana ambao wamekatisha masomo kutokana na ujauzito akiwemo Neema Gervas, walisema baada ya chama cha wakunga Tanzania TAMA, kuwapa elimu wametambua namna ya kulea watoto wao na kujitambua, huku wakitaka kuwepo kwa mkazo zaidi wa kisheria ili kuwaepusha wasichana na mimba za mapema.

"Sheria zikisimamiwa na watuhumiwa kuwa wanapewa adhabu kwa mujibu wa Sheria hizo basi mimbo kwa wasichana zitatokomezwa lakini kama watuhumiwa hawatachukuliwa sheria basi vitendo vya kubebesha mimba wasichana havitaisha" alisema Neema. 

Kwa mujibu wa Mratibu wa Afya ya Uzazi kutoka  Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu Duniani, UNFPA Dkt.Sunday Rwebangira alisema asilimia 32% ya wasichana katika mkoa wa Kigoma hupata ujauzito katika umri mdogo.

"Tulipokuja Kigoma tulikutana na changamoto nyingi ambazi vijana wanazipata ikiwemo wasichana kubeba ujauzito katika umri mdogo" alisema Dkt Sunday. 

Mwisho
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com