METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 16, 2019

MWENYEKITI TUGHE PWANI AFANYA ZIARA BAGAMOYO KUSIKILIZA NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAFANYAKAZI





MWENYEKITI wa Chama Cha wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) wa Mkoa wa Pwani Ameanza Ziara ya Kutembelea Taasisi Mbalimbali za Wilaya ya Bagamoyo ambapo Kuna Wafanyakazi Ambao ni Wanachama Wao kwenye Chama Hicho kwa Ajili ya Kuwasikiliza,Kupokea Changamoto zao na Kuzitatua Pale Inapobidi kwa Haraka Zaidi. 

Akizungumza na wafanyakazi wa taasisi ya sanaa Bagamoyo (Tasuba) baada ya kuwatembelea Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Pwani,Catherine Katele alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kutoa semina fupi juu ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) jinsi unavyofanya kazi zake katika kuwahudumia watumishi wa umma lakini pia kusikiliza kero na changamoto za wafanyakazi hao na kuzichukua kuzifikisha sehemu husika pamoja na kuwashukuru kwa kumchagua kuwa kiongozi wao kwa kipindi cha miaka mitano. 

“Tangu nimechaguliwa nafasi hii sikuwahi kuja kuwatembelea ndugu zangu watumishi wenzangu wa serikali japo kuwashukuru kwa kunichagua kwa kura za kishindo lakini pia sikuja bure nimeongozana na wenzangu kutoka ngazi ya mkoa ambapo leo hii mtanufaika kwa kupata semina fupi juu ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) jinsi unavyofanya kazi katika kumsaidia mtumishi wa umma pindi anapopatwa na matatizo akiwa kazini pamoja na kusikiliza kero na changamoto zenu tuzibebe na tuzifikishe sehemu husika zishughulkikiwe; 

“Kwa sasa katika taasisi nyingi kumekuwa na hali ya sintofahamu ambayo inaleta mkanganyiko katika kipindi cha kutoa mfanyakazi bora mfano katika taasisi yenu hii kuna wafanyakazi ambao wapo katika vyama vingine vya wafanyakazi ukiachia chama chetu cha tughe sasa muda ukifika badala ya kuangalia mfanyakazi gani ameiletea taasisi mafanikio kinachoangaliwa kila watumishi na vyama vyao wanavutia upande wao,mimi niseme hatuendi hivyo niwasihi tumchague mfanyakazi kwa manufaa aliyoiletea taasisi yake na ubora wa utendaji kazi wake” Alisema Mwenyekiti Katele. 

Aidha Mwenyekiti Katele amewaambia uongozi wa tawi la Tughe katika taasisi ya Tasuba kuwa Viongozi wamehakikisha wanasimamia haki za wanachama wao kwa kuhakikisha asilimia 20% zao za matawi zinaanza kutolewa na madeni Yote ya Nyuma yanalipwa. 

Hata Hivyo Katibu wa Tughe wa Mkoa wa Pwani,Shadrack Mkodo wakati akitoa semina kuhusu mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) kwa watumishi hao wa Tasuba aliwaambia kuwa kazi inaanzia unapotoka mlangoni kwako au getini unaanza kuhesabika upo kazini hadi unafika ofisini unasaini hadi muda wa kuondoka hadi unafika nyumbani kwako lolote litakalokutokea utahesabika umepatwa na tatizo hilo ukiwa kazini ila endapo utakutwa na tatizo ukiwa umekwenda sehemu nyingine tofauti na maelekezo ya kazi yako inavyosema utakuwa umepatwa na matatizo hayo nje ya kazi akatolea mfano kama ukiumia bar na kumbi za starehe. 

Naye mmoja kati ya wafanyakazi wa Tasuba ambaye ni mwanachama wa tughe, Mkufunzi, Haji Maeda aliwashukuru uongozi wa chama cha wafanyakazi kwa mkoa wa pwani kufanya ziara hiyo ambayo kwa namna moja itasaidia kutatua kero na changamoto zao walau kwa kiasi na kuwaomba kuwatembelea mara kwa mara ili kuzidi kuwasaidia katika kutatua matatizo yanayowakabili pamoja na kuwapatie elimu juu ya stahiki na haki zao kama wafanyakazi. 

Katika msafara wa Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) Mkoa wa Pwani ambao ulikuwa ukiongozwa na Mwenyekiti wake,Catherine Katele na Katibu wake,Shadrack Mkodo pia uliambatana na Mwakilishi wa Vijana Mkoa wa Pwani Tughe,Dk.Christian Benedict,Katibu wa Tughe Mkoa wa Dar es Salaam,Litson Magawa,Mratibu Tughe Wilaya ya Bagamoyo,Timothy George Twalib,Mratibu Tughe Wilaya ya Kibaha,Dk.Baraka Makayo.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com