Wazari wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
AGIZO la Rais John Magufuli kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto la kuhakikisha halmashauri zote nchini zinachukua dawa za viuadudu zinazozalishwa kwa katika kiwanda cha dawa hizo kilichopo Kibaha, Pwani, limeanza kutekelezwa kwa halmashauri 14 kutakiwa kufika katika kiwanda hicho na kuchukua dawa hizo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo akiwa katika hafla ya uzinduzi wa Barabara ya Bagamoyo – Makofi – Msata wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani iliyoanza Juni 21 hadi 23, 2017, alipotoa siku saba kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha zinachukua dawa hizo.
Alilipia lita 100,000. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto -Idara Kuu ya Afya, Catherine Sungura, viuadudu hivyo vitaanza kugawiwa katika halmashauri za mikoa 14 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria.
“Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anapenda kuwatangazia Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuwa viuadudu vitaanza kugaiwa Juni 26, 2017 (Juzi Jumatatu) kwa halmashauri za mikoa 14 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa Malaria,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo mikoa inayoanza kupata mgao huo, na viwango vya maambukizi ya malaria kwenye mabano katika asilimia ni Kagera (41), Geita (38), Kigoma (38), Ruvuma (23), Tabora (20), Mtwara (20), Mara (19), Shinyanga (17), Lindi (17), Pwani (15), Mwanza (15), Katavi (14), Morogoro (14) na Simiyu (13).
Taarifa ilisema mikoa ambayo haijatajwa itagawiwa viuadudu katika awamu nyingine. Aidha taarifa hiyo imewakumbusha waganga wakuu wa mikoa na wilaya kufanya upuliziaji wa viuadudu kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya. Hii itawezesha kupata matokeo tarajiwa ya kutokomeza mbu ili kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini.
“Wizara ya Afya inapenda kumshukuru kwa dhati na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuongeza chachu katika mapambano dhidi ya malaria nchini,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
0 comments:
Post a Comment