Serikali
imeainisha maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2017/2018 kulingana na
mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka ujao wa fedha.
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alisema hayo jana Bungeni mjini
Dodoma alipokuwa akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa
Taifa 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2017/2018.
Dkt.
Mpango alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na miradi ya kielelezo
ya maendeleo ambayo inayolenga kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ni pamoja na miradi ya Makaa ya Mawe
Mchuchuma, Mchuchuma Liganga, ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es
salaam, Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa km 1,251 kwa “Standard Gauge”
pamoja na matawi yake ya Tabora kupitia Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa
km 379, Isaka hadi Rusumo km 371, Kaliua kupitia Mapanda hadi Karema km
321, Keza hadi Ruvubu km 36 na Uvinza hadi Kelelema kuelekea Musongati
yenye urefu wa km 203.
Miradi
mingine ya kielelezo ni uboreshaji wa Shirika la Ndege TAanzania (ATC),
ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi mkoani Lindi, uanzishwaji wa Kanda
Maalum za Kiuchumimkoani Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma, uanzishwaji wa
kituo cha biashara cha Kurasini, kusomesha vijana katika stadi za
mafuta na gesi, uhandisi na huduma za afya.
Waziri
Dkt. Mpango aliyataja maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni viwanda vya
kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa kukuza uchumi wa viwanda,
kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu, mazingira ya
wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, ubia kati ya sekta ya umma
na sekta binafsi pamoja na maeneo mengine muhimu kwa ukuaji wa uchumi
na ustawi wa taifa.
Dkt.
Mpango alisema kuwa shabaha ya uandaaji wa mpango wa bajeti ya mwaka
2017/18 unaongozwa Serikali kusimamia mambo ya uchumi kwa ujumla ikiwemo
kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la taifa kufikia asilimia 7.5
kwa mwaka 2017, asilimia 7.9 mwaka 2018 na asilimia 8.2 mwaka 2019,
kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo
wa tarakimu moja kufikia asilimia 5.0 katika kipindi cha muda wakati,
kuwa na pato ghafi la taifa la sh. trilioni 123.9 kwa mwaka 2017/18, sh.
trilioni 139.7 kwa mwaka 2018/19 na sh. trilioni 165.4 mwaka 2019/20
pamoja na mapato ya kodi kufikia asilimia 14.6 ya pato la taifa mwaka
2017/18, asilimia 15.5 mwaka 2018/19 na asilimia 15.8 mwaka 2019/20.
Aidha,
alitaja misingi ya mpango na bajeti kuwa ni amani, usalama, utulivu na
utangamano wa ndani ya nchi na nchi jirani ambavyo vitaendelea
kudumishwa nchini.
Kuhusu
mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018,
Dkt. Mpango alisema amewaagiza Maafisa Masuuli kuzingatia masuala muhimu
wakati wa uandaaji wa mipango na bajeti za mafungu yao ili kutekeleza
Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015.
Zaidi
ya hayo, Dkt. Mpango alisisitiza uwepo usimamizi na udhibiti wa
matumizi, ulipaji na ongezeko la madeni ya Serikali, ukusanyaji wa
mapato pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za utekelezaji.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Hawa Ghasia
alipokuwa akitoa taarifa ya kamati yake alisema kuwa Kamati yake
inardhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kusimamia Sheria
ya Bajeti na kanuni zake ambayo inahakikisha usimamizi na uwajibikaji
katika hatua zote za mchakato wa bajeti unazingatiwa.
Naye
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Halima Mdee alipokuwa
akiwasilisha hotuba yake alisema kuwa Kambi Rasmi inaunga mkono hatua za
kisheria zinazochukuliwa na Serikali kwa wale wote waliohusika kwa
namna moja au nyingine kuhujumu uchumi wa nchi.
Mkutano
wa Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajiwa
kuhitimishwa Novemba 11 mwaka huu huku shughuli mbalimbali za kuishauri
Serikali zikiwasilishwa kupitia mijadala ya Wabunge.
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma
0 comments:
Post a Comment