Neema
Lema (33), mke wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema),
amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Alifikishwa
mahakamani hapo jana na kuunganishwa katika kesi ya tuhuma za kusambaza
ujumbe unaomkashifu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Katika
kesi hiyo ya jinai namba 351 ya mwaka huu, mshitakiwa mwingine ni Lema
ambaye alifikishwa mahakamani hapo Agosti 20 mwaka huu.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Agustine Rwizile, Wakili wa
Serikali, Blandina Msawa, aliiomba mahakama kufanya marekebisho kwenye
hati ya mashtaka kwa kumuongeza Neema.
Akisoma
mashtaka yanayomkabili Neema, wakili huyo alidai Agosti 20 mwaka huu,
jijini Arusha, mshtakiwa alituma ujumbe kwa simu ya mkononi uliosema, ‘karibu tutakudhibiti kama Uarabuni wanavyodhibiti mashoga’.
Neema
anayetetewa na Wakili Sheck Mfinanga, alikana kutenda kosa hilo na
kupewa dhamana hadi Novemba 15, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Wakati
huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Arusha, lilimkamata na kumhoji Lema kwa
tuhuma za kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles
Mkumbo, alisema Lema alitoa lugha hiyo wiki iliyopita katika mikutano
halali aliyoifanya jimboni kwake.
“Tumemkamata Lema kwa kutoa lugha ya uchochezi ambayo ni kinyume cha sheria.
“Baadhi ya maneno aliyotoa yenye uchochezi ni pamoja na kusema Rais
Magufuli akiendelea kugandamiza demokrasia, taifa litaingia katika
umwagaji wa damu, nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa
udikteta pamoja na kuwataka wananchi wawe tayari kwa lolote na waache
uoga kwa vile uoga ni dhambi mbaya kuliko dhambi zote duniani.
“Baada
ya kumhoji kuhusu maneno hayo, tulimwachia kwa dhamana na sasa jalada
lale liko kwa Mwanasheria wa Serikali kwa ajili ya kuandaa hati ya
mashitaka afikishwe mahakamani,” alisema Kamanda Mkumbo.
0 comments:
Post a Comment