Ndugu Viongozi na wanachama wa CCM kwa umoja wetu tumelazimika kukusanyika mahali hapa kwa kazi moja muhimu ikihusiana na chimbuko la historia ya nchi yetu tokea tulipopata uhuru Disemba 9 mwaka 1961 na pale yaliofanyika Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Januari 12 mwaka 1964.
Tokea tupate uhuru Taifa letu lilikumbwa na misukosuko kadhaa ikiwemo mikwamo na mitikisiko ya kiuchumi.
Kwa bahati nzuri sana jana Tarehe 24 Mei 2017 limefanyika tukio jingine kubwa la kihistoria ambalo nalo linalohitaji kuingizwa kwenye kurasa za kumbukumbu muhimu ya nchi yetu.
Tokea tujikomboe, kuunganishwa kwa mataifa yetu ya Tanganyika na Zanzibar, kujitawala sisi wenyewe , miaka yote tumekuwa tukihubiri juu ya dhamira ya kuheshimu misingi ya utaifa na uzalendo.
Viongozi wetu na maandiko mbalimbali yamehimiza kuhusu matumizi bora ya Rasilimali za Taifa na Maliasili asili zilizopo. Tumehimizana juu ya kujenga Umoja wa kitaifa, kupigania haki, usawa, kukataa ukabila na kudumisha amani chini ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Katika awamu ya kwanza ya utawala wa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kulianzishwa Viwanda vingi, kampuni za Serikali na mashirika ya umma.
Nchi yetu ilipiga hatua kubwa mbele ya mataifa mengine Afrika Mashariki na Afrika kiuchumi kwa sababu ilimudu kuzalisha bidhaa zake na kuuza ndani na nchi za nje huku ikipata fedha za kigeni.
Ndugu Vijana wenzangu
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani Karume, walikuwa na malengo mazuri, mipango na mikakati ya kuzijenga nchi zao kiuchumi lakini kwa bahati mbaya baadhi ya watanzania waliokabidhiwa dhamana za uendeshaji na usimamizi, walipungukiwa na shime ya uzalendo na kujikuta karakana, Viwanda, Taasisi na Mashirika yalioanzishwa kwa nia njema yakifilisika.
Hata hivyo waliohusika katika kufilisi mashirika hayo ya Umma , Viwanda na kampuni za Serikali kwa namna moja au nyingine, hawakuchukuliwa hatua na wala wahusika wake kufikishwa katika vyombo vya sheria kujibu jambo lolote.
Pamoja na juhudi kubwa za uanzishaji wa viwanda na mashirika ya umma ambayo yalikuwa yakizalisha bidhaa muhimu,nchi yetu ikajikuta ikirudi hatua nyingi nyuma za kiuchumi na kimaendeleo kwa sababu ya kukosekana usimamizi makini, uwajibikaji, uwazi na kutolidhibiti kundi la mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma dhidi ya watu waliotamani kujivika mataji ya ubepari na unyonyaji.
Hata hivyo haikushuhudiwa aina ya viongozi walaji Serikalini , wakwapuzi na wabadhirifu wa mali za umma au mafisadi aidha katika awamu ya kwanza, pili na ya tatu wakishitakiwa hadi pale kwa mara ya kwanza katika awamu ya nne vigogo watatu waandamizi wa serikali walipofikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa kushitakiwa na hukumu kutokewa kwa mujibu wa sheria
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi unafikiri na kuamini kuwa udhaifu au kulegalega kwa vyombo husika na dhamana hadi kushindwa kuchukua hatua za kisheria katika kukabiliana na ubadhirifu wa mali za umma uliofanywa na wezi, wabadhirifu na mafisadi, kumechangia kwa kiasi kikubwa kulifikisha Taifa letu mahali pabaya kiuchumi hatimaye hata wanyama kama Twiga na Faru wakipandishwa kwenye ndege kwenda ughaibuni .
Maendeleo ya kila Taifa aghalabu hutegemea vyanzo vyake vya ndani kwa maana ya vitega uchumi vyake, maliasili zake na rasilimali kadhaa ikiwemo mitaji itokanayo na Viwanda, Mashirika, kampuni za Serikali, wanyama, mbuga, madini, utalii na fursa nyingine muhimu za kisekta.
Kwa miaka mingi vyanzo vyote hivyo muhimu vilipokuwa vikizalisha, tija na faida zake zimewanufaisha watu wachache. Wananchi wengi hasa walioko vijijini wamekuwa wakikosa huduma bora za kijamii huku familia za wezi na mafisadi zikiishi maisha ya anasa, fahari na kibwenyenye.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tunadhani kuwa vipindi na zama hizo zimepita na pengine hazitarudi tena. Sasa kuna zama mpya ambayo ni makini, inayotazama haki na maslahi ya umma, ikitazama shida za wananchi na kupigania maendeleo yao.
Ndugu Vijana wenzangu;
Ikumbukwe kuwa tokea akiwa katika ngwe ya kampeni za kuwaomba ridhaa wananchi ili aliongoze Taifa letu, Rais Dk John Magufuli aliahidi huku akisema chini ya Serikali yake itakayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, maliasili na rasilimali zote za nchi zitawanufaisha wananchi wenyewe na kamwe hazitakwenda katika matumbo na mikono ya mafisadi na wezi.
Umoja wa Vijana wa CCM tumeamua kutoka mbele ya hadhara kuelezea kuridhishwa kwetu na hatua stahiki anazozichukua Rais Magufuli huku akizingatia maelekezo na maagizo aliyopewa na Chama Cha Mapinduzi kwenda kuyasimamia Serikalini.
Kazi anayoifanya Rais Magufuli ndiyo kazi tuliyomtuma wana CCM wapenda amani, wazalendo na wakereketwa wa maendeleo ya Taifa letu la Tanzania.
Hakuna jambo geni na alilolianzisha mwenyewe Rais Magufuli isipokuwa yote ni maelekezo yanayotokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015 - 2020.
Wale wanaobeza na kusema eti CCM kazi yake kufuga wezi tunawaambia wezi, mafisadi, na wala rushwa CCM sio sehemu yao na ndio maana hawadumu ndani ya Chama na kwenye Serikali yoyote inayoundwa na Chama Cha Mapinduzi.
Jambo hili kubwa alilolifanya Dkt. Magufuli kwa masilahi ya Taifa limezungumzwa na kuwekewa msisitizo katika Ilani ya Uchaguzi mwaka 2015/2020 nanukuu
(i) “Kusimamia na kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini ili kukuza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa”
(k) “Kubuni na kutekeleza mikakati mahsusi itakayowezesha kupunguza au kukomesha kabisa vitendo vya utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na biashara haramu ya madini nchini”.
Mapema tarehe 29 March mwaka 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliunda Tume ya uchunguzi wa mchanga wa madini ili kujua ni kiasi gani Taifa linapoteza bila kunufaika. Tume hiyo ikapewa hadidu za rejea ili kukamilisha kazi hiyo kwa weledi, uwazi na kuipatia serikali majawabu ya kutosha.
Hivyo kwa maelezo hayo Umoja wa Vijana wa CCM unaunga mkono ripoti ya Kamati, matokeo ya uchunguzi na mapendekezo yake hivyo kwa kauli moja Vijana tunatamka ifuatavyo:-
TAMKO LA UVCCM BAADA YA RIPOTI YA TUME :
• Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tunampongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa na uzalendo wa hali ya juu alionao kwa Taifa.
• Umoja wa Vijana wa CCM tunaunga mkono maamuzi yote yaliyopitishwa au kutolewa na Rais Dk John Magufuli mara baada ya kupokea ripoti ya Tume ya Uchunguzi
• Umoja wa Vijana wa CCM hutuko tayari na hatutakubali kushuhudia tena Tanzania ikirejea katika zama ya kiza kinene cha ukwapuaji mali, ulaji, kufilisi mashirika ya umma au wizi wa mali za umma.
• Umoja wa Vijana wa CCM tunaishauri serikali yetu iendelee na mikakati yake ya kuhakikisha ukwapuaji, ubabaishaji, wizi na ufisadi wa mali za serikali vinavikomeshwa mara moja
• Umoja wa Vijana wa CCM tunaiomba kwa dhati Serikali yetu ianze kuipitia upya mikataba yote ya madini ili kubaini kama ni yenye manufaa na maslahi mapana kwa umma .
• Umoja wa Vijana wa CCM tunamuomba Rais Dk John Magufuli kuwaweka pembeni wasaidizi wake wote ambao bado wanaonekana kuwa na kigugumizi katika kuwatumikia wananchi huku baadhi yao wakiona muhali kupambana na ufisadi.
• Umoja wa Vijana wa CCM tunasisitiza kuwa Watendaji wote waliokuwa na dhamana na ambao wamehusika kwa namna moja au nyingine kupoteza mapato na kulitia hasara Taifa, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao haraka .
• Umoja wa Vijana wa CCM tunaishauri Serikali kuendelea kuwabaini na kuwachukulia hatua Viongozi na watendaji wa serikali ambao watabainika kumiliki mali, utajiri na vitega uchumi ambavyo havitokani na mapato yasiolingana na vipato vyao wataifishwe kama ilivyofanyika mwaka 1967 baada ya kutangazwa Azimio la Arusha .
• Umoja wa Vijana wa CCM tunaishauri serikali kuendesha shughuli zake za kiutawala kwa kusimamia, kuongozwa na kufuata miiko na maadili ya uongozi kama yalivyotajwa na kuelekezwa katika Azimio la Arusha kwa sababu Azimio hilo lipo hai kisheria na bado halijafa.
• Vijana wote tunaishauri serikali yetu isikubali na isiafiki mali za umma zitumike kwa maslahi binafsi badala yake kila miliki ya serikali na mali ya umma ifahamike kuwa kila mwananchi ana haki kufaidika nayo ambayo ni sehemu ya matunda ya Uhuru na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Aidha Umoja wa Vijana wa CCM unawataka wana CCM na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na Serikali yake katika mapambano dhidi ya vikundi vya rushwa, ufisadi na uzembe kwa baadhi ya watendaji ili kuleta maendeleo endelevu katika taifa letu. Mwisho Umoja wa Vijana wa CCM tunaahidi tutamlinda, tutamtetea kwa gharama yoyote Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM kwa kutekeleza mambo yote mema ambayo tunaamini yataleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Vijana tumeendelea kuwa na imani kubwa na Ndugu John Joseph Magufuli kuwa changamoto nyingi za Vijana kumalizakia zinawezekana kwa kuimarisha Uchumi kwanza ili Vijana waweze kufanya kazi kupitia rasilimali za nchi yetu. Wito kwa Vijana wenzetu hakuna kukata tamaa sasa ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii mwanga wa matumaini umeonekana sura mpya ya taifa linaweka katika mageuzi makubwa ya kiuchumi imeonekana.
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
0 comments:
Post a Comment