Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, bungeni mjini Dodoma Aprili
10, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo wa Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Bw. Shenal Nyoni ili kupisha uchunguzi wa tuhuma
zinazomkabili kwa kuongeza gharama za pembejeo kwa kushirikiana na
baadhi ya mawakala wa pembejeo za kilimo.
Amesema Serikali italipa madeni yote ya
mawakala wa pembejeo za kilimo mara baada ya kukamilisha uhakiki na
kujiridhisha juu ya uhalali wake, sababu bado inawahitaji mawakala ili
kushirikiana nao katika kuhudumia wakulima kwenye maeneo mbalimbali
nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumatatu, Aprili 10, 2017) katika kikao alichokiitisha kwenye Makazi ya
Waziri Mkuu mjini Dodoma kati yake na mawakala wa pembejeo za kilimo
pamona na Maofisa kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Gharama ya madeni ni kubwa kuliko
pembejeo zilizosambazwa. Hii inatokana na udanganyifu mkubwa unaofanywa
na mawakala kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali wanaohusika na
masuala ya pembejeo,”
Amesema kuwa kwenye eneo la pembejeo
kuna matatizo makubwa kutokana na baadhi ya Maofisa kuzungumza na
mawakala na kuongeza gharama za pembejeo kwa lengo la kuibia Serikali na
kisha kugawana fedha. “Sasa Serikali haiwezi kulipa madeni ya
kutengenezwa bali tutawalipa stahili zenu baada ya uhakiki kukamilika
kama nilivyosema awali,”.
Waziri Mkuu ameongeza mawakala wa
pembejeo waliwasilisha Serikali deni la sh. bilioni 65.4 kwa huduma
waliyoitoa katika mikoa 25 ambapo Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
imekamilisha uhakiki wa madeni hayo kwa mikoa 10 ya Morogoro, Iringa,
Njombe, Ruvuma, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha
ambayo madeni yake ni asilimia 70 ya madeni yote.
Amesema ripoti ya uhakiki wa mikoa nane
kati ya 10 imetoka (imebaki Katavi na Kigoma) na kubainisha kuwa mikoa
hiyo inadai sh. bilioni 36 kati ya hizo sh. bilioni 11 bado zinaendelea
kuhakikiwa, sh. bilioni 14 zimekataliwa hivyo siyo madeni halali, sh.
bilioni 8.2 ndiyo deni halali na sh. bilioni 2.3 zinachungizwa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Waziri Mkuu amesema uhakiki wa madeni
kwa mikoa 15 iliyobakia ambayo madeni yake ni asilimia 30 unaendelea
ambapo amewasihi mawakala hao kuwa wavumilivu katika kipindi ambacho
Serikali inafanya uhakiki kwa kuwa inataka itende haki kwa kila mtu
kulipwa deni lake kwa kiwango kinachostahili na watakaobainika kufanya
udanganyifu watachukuliwa hatua za kisheria.
0 comments:
Post a Comment