NA HAMZA TEMBA – WMU
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof.
Jumanne Maghembe ametangaza mabadiliko makubwa katika biashara ya mkaa
nchini na kusema kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu hakuna mkaa wowote
utakaosafirishwa kutoka wilaya moja kwenda nyingine ili kunusuru misitu
inayoteketea kwa kasi hapa nchini.
Amesema hayo leo wakati akifungua
mkutano wa 24 wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii
uliofanyika katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe
mbalimbali kutoka kwenye Idara, Vitengo na Taasisi mbalimbali zilizopo
chini ya Wizara hiyo.
“Kuanzia mwezi Julai hakuna ruhusa ya
kutoa vibali vya kuhamisha mkaa kutoka wilaya moja kwenda wilaya
nyingine, mkaa utachomwa, utauzwa ndani ya wilaya kwa ajili ya matumizi
ya watanzania wanaohitaji nishati ya mkaa, lakini biashara ya mkaa ya
kutoa Dodoma kwenda Dar es Salaam mpaka Zanzibar marufuku.
“Wamekata misitu yetu yote, mito yetu
imekauka, tunashindwa kupata maji ya umwagiliaji kwasababu watu wengi
huko nje wanataka mkaa wetu, Tanzania jamani sio shamba la bibi, wale
wote watakaotoa mkaa kutoka eneo moja hadi jingine kinyume na sheria hii
watashuulikiwa kwa utaratibu wa uhujumu uchumi”, amesema Maghembe.
Amesema kuwa kwa upande wa miji mikubwa
kama Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na Tanga vitaanzishwa viwanda
maalumu vya kuzalisha mkaa ambao utauzwa kwa vibali maalumu katika mikoa
mbalimbali hapa nchini. Amesema mkaa huo hautakuwa na athari nyingi za
kimazingira kwa sababu utazingatia taratibu za uzalishaji endelevu.
Wakati huo huo, Waziri Maghembe
amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
kumuhamisha kituo cha kazi Mkuu wa Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia
Uharibifu wa Misitu wa Wakala hiyo, Arjason Mloge kutoka Makao Makuu ya
Taasisi hiyo kwenda chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) kilichopo mkoani
Kilimanjaro na badala yake atafutwe mtu mwingine muaminifu.
Amesema uamuzi huo ni kufuatia udhaifu
uliojitokeza katika usafirishaji wa rasilimali za misitu ndani na nje ya
nchi ikiwemo usafirishaji kwa kutumia nakala za vibali ambazo sio
halisi, yaani “Photocopies”. “Agizo hili litekelezwe mara moja kabla ya
saa sita mchana wa leo na niwe nimepewa nakala ya barua hiyo ya
uhamisho” amesema.
Kufuatia uamuzi huo amepiga marufuku
kuanzia leo usafirishaji wa mazao ya misitu ndani na nje ya nchi kwa
kutumia nakala zisizo halisi (Photocopies). Ameongeza kuwa katika kuunga
mkono Sera ya Uchumi wa Viwanda ya Serikali ya awamu ya tano hakuna
gogo litakalosafirishwa kwenda nje ya nchi.
“Wawekezaji wanahimizwa kujenga viwanda
vya kuchakata magogo hayo hapa nchini ili kutoa ajira kwa Watanzania
pamoja na kutoa faida halisi inayotokana na rasilimali hizo kwenye
uchumi wa taifa”, amesema.
Akizungumzia changamoto ya mifugo kwenye
maeneo ya hifadhi nchini amesema Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5
ya mwaka 2009 sehemu ya 21 (1) hairuhusiwi kabisha kuchunga mifugo
katika Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za
Misitu. Amewataka watumishi wa Maliasili kusimamia Sheria hiyo pamoja na
kutoa wito kwa wananchi kuifuata kikamilifu.
Katika hatua nyingine, Waziri Maghembe
amewataka majangili wote nchini kuachana na biashara hiyo haramu ambayo
hailipi kwa sasa na badala yake wachukue matrekta wakalime.
“Mtu ambaye alikuwa anaishi kwa
kutegemea ujangili sasa atafute trekta akalime, kwa sababu akifanya
ujangili tukamkamata tu, na tukimkamata atakaa kwenye hoteli ya mkuu wa
magereza (magereza) kwa zaidi ya miaka 25”.
Aidha, Waziri Maghembe ametoa pongezi
kwa watumishi wote wa Wizara ya Maliasili kwa kazi nzuri wanayofanya ya
kupambana na ujangili nchini pamoja na ulinzi wa maliasili za taifa
(Misitu, Wanyamapori na Mambo ya Kale) ambazo kwa pamoja zinachangia
asilimia 20.5 kwenye pato la taifa. Amesema matokeo chanya ya kupambana
na ujangili yameanza kuonekana japo ujangili bado upo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki amemueleza Waziri Maghembe kuwa maelekezo
yote aliyoyatoa yamepokelewa kwa ajili ya kuyafanyiwa kazi, huku Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexandre Songorwa akimueleza
Waziri huyo kuwa watalinda na kusimamia Malisili za Taifa na kwamba katu
hawapo tayari kuandikwa kwenye vitabu kuwa walishiriki katika kutoweka
kwa maliasili hizo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Maghembe (katikati) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa
24 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo terehe 10
Aprili, 2017 katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma. Kushoto ni Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki na Mwenyekiti wa Baraza hilo,
Esther Malima.
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa
Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (katikati waliokaa) na
wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo baada ya
kufungua mkutano huo leo terehe 10 Aprili, 2017 katika ukumbi wa LAPF
mjini Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 24
wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo terehe 10
Aprili, 2017 katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhandisi Ramo Makani (katikati) akiimba wimbo wa Umoja wa Wafanyakazi
(Solidarity Forever) muda mfupi kabla ya kufunga mkutano huo leo terehe
10 Aprili, 2017 pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali
Gaudence Milanzi (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa Baraza hilo, Esther
Malima (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof.
Alexandre Songorwa (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala
na Rasilimali Watu, Mrimia Mchomvu.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili
na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki (wa pili kshoto) akizungumza katika mkutano
huo leo terehe 10 Aprili, 2017.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza
la Wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakisikiliza hotuba ya
ufunguzi wa baraza hilo kutoka kwa Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Jumanne
Maghembe (hayuko pichani) katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma leo.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe na wageni waalikwa katika mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe katika mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe na wageni waalikwa katika mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti.
Baadhi ya wajumbe Sekretarieti wakiteta jambo nje ya ukumbi.
0 comments:
Post a Comment