Na Hassan Silayo-MAELEZO
Kuanzia 02 Machi, 2017 Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alianza ziara ya kikazi
ya siku 4 katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara iliyolenga kutembelea
miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika mikutano
ya hadhara.
Ziara hiyo kwa kiasi kikubwa imeonesha
dira na mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano hasa katika utekelezaji wa
miradi inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali Imani,kabila
na itikadi za vyama vyao vya siasa.
Siku ya kwanza ya ziara yake Rais Dkt.
Magufuli aliweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles)
cha Tanzania Goodwill Ceramic Tiles Ltd. kilichopo Mkuranga Mkoani
Pwani ambacho ni kikubwa Afrika Mashariki na Kati kilichogharimu Dola za
Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza.
Akiongea katika hafla ya uwekaji wa jiwe
la msingi katika kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000
za vigae kwa siku Rais Magufuli alifurahishwa na teknolojia ya
kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae inayotumiwa na kiwanda hicho na
kuhoji kama kuna haja ya serikali kuendelea kusafirisha mchanga wa
madini nje ya nchi.
Rais Magufuli alisema kuwa “Nchi hii
tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa
kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga
nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto
1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya
Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje
ya nchi”
Akiwa njiani kuelekea Mikoa ya Lindi na
Mtwara Rais Magufuli alizungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero
zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi
wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya
Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi wa tatu
na kupiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo
wa mazao.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli anawataka
wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha
kutosha katika kipindi hiki mvua zinaponyesha huku akiweka bayana kuwa
Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali
wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.
Akioneshwa kutoridhishwa na utekeleaji
wa miradi inayogusa maisha ya wananchi alipotembelea ujenzi wa mradi wa
maji wa Ng’apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe
17 Machi, 2015 Rais Magufuli aliagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria
za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas Infranstructure
Alliance Private Limited ya India Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi
wake mpaka hapo kampuni hiyo itakapokamilisha mradi huo unaotarajiwa
kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya
wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.
Katika kuthibitisha amedhamiria kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda Rais Dkt. Magufuli aliitaka Wizara ya
Nishati na Madini Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha
gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo lengo likiwa kuondoa
vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa
vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama mara kwa mara.
Aidha, Dkt. Magufuli aliitaka Wizara
hiyo kuhakikisha wanamega eneo lenye makaa ya mawe katika eneo la Ngaka
lililopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni ya Dangote
ili iweze kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha
saruji kilichopo Mkoani Mtwara.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Alhaji
Aliko Dangote tangu kianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo sokoni
imeshuka kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi
kufikia Shilingi 10,000/- na ununuzi wa magari 580 yatasaidia
kusafirisha saruji nchi nzima kwa gharama nafuu ambayo watanzania wengi
wataimudu.
Wakati akikamilisha Ziara yake Mhe.
Dkt. Rais Magufuli alifanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa
Mjini Mtwara ambapo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga
kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Nchi kwa nguvu kubwa kwa manufaa ya
wananchi.
Rais Magufuli alisema kuwa Serikali ya
awamu ya tano imedhamiria kutilia mkazo juhudi za uendelezaji wa bandari
ya Mtwara, ujenzi wa barabara, uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya
umeme, ujenzi wa viwanda vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za
kilimo ambavyo vitasaidia kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha
maisha ya watu.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli alioneshwa
kusikitishwa na Mkoa wa Mtwara kufanya vibaya kielimu na kuwataka kuweka
msisitizo katika elimu kwani juhudi za Serikali kuwapelekea maendeleo
hazitakuwa na maana kama wananchi watakuwa hawana elimu.
Ziara hiyo ya Rais Dkt. Magufuli
imeonesha mwelekeo wa Tanzania tunayoitaka hasa katika maeneo ya
usimamizi wa miradi na utekelezaji wake kwa maslahi ya umma.
0 comments:
Post a Comment