Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)
imekanusha juu ya uvumi unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu
uuzaji wa viwanja katika eneo ka Mkonze lililopo mkoani Dodoma.
Tamko hilo limetolewa hivi karibuni
mkoani Dodoma na Kaimu Meneja Uhusiano wa CDA, Angela Msimbira kutokana
na kusambaa kwa ujumbe huo katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Bi. Angela amesema taarifa hizo ambazo
hazieleweki zimekuwa zikidai kuwa viwanja hivyo ni halali na ukinunua
unapewa hati na CDA ambayo ndiyo imepewa dhamana ya ugawaji wa viwanja
mkoani humo.
“Mamlaka yetu inapenda kuutarifu Umma
kuwa taarifa hizo si za kweli hivyo wananchi wanatakiwa kuzipuuza na
kuendelea kufata utaratibu kwani mamlaka hiyo ina utaratibu uliopangwa
wa namna ya kupata viwanja vilivyo halali,”alisema Bi. Angela.
Amefafanua kuwa Mamlaka hiyo inapotaka
kuuza viwanja hutumia utaratibu wa kutangaza kwenye vyombo vya habari,
mitandao ya kijamii pamoja na kutoa matangazo kwa umma kwa njia ya
vipaza sauti.
Aidha, Bi. Angela ametumia fursa hiyo kuendelea kuwakumbusha wananchi kufuata taratibu za upatikanaji wa viwanja.
Kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria
ya Makosa ya Jinai Mitandaoni ya mwaka 2015, ni kosa kwa mtu yoyote
kutangaza, kuchapisha au kueneza habari za uongo au uzushi katika
mitandao.
0 comments:
Post a Comment