METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 14, 2017

Tume yasikitika Rahco kuvunja nyumba Buguruni

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesikitishwa na kitendo kilichofanywa na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco) kubomoa nyumba zaidi ya 200 zilizojengwa pembezoni mwa reli eneo la Buguruni, Machi 11, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga, kampuni hiyo ilitekeleza ubomoaji huo, wakati ikiwa na taarifa ya mwito wa Tume kuhusu malalamiko ya wananchi wa eneo hilo.
Malalamiko hayo yanahusu uhalali wa makazi yao kuwa nje ya mita 15 au mita 30 kama Sheria ya Reli Namba 4 ya Mwaka 2002, inavyoelekeza.

“Ubomoaji wa nyumba hizi ulianza tangu Machi 11 saa nne asubuhi katika Mtaa wa Madenge, Kata ya Buguruni na uliendelea Machi 12, mwaka huu katika mitaa ya Faru, Mtakuja na Mtambani katika kata ya Mnyamani,” alisema Nyanduga.

Alisema Februari 22, mwaka huu, Kamati iliyoundwa na wananchi wa Mnyamani ilifika katika Ofisi za Tume na kusajili lalamiko lao kwamba nyumba zao ziliwekwa X kuashiria kuvunjwa bila wao kujulishwa.

Alisema baada ya malalamiko hayo, Tume iliwasiliana na uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mtambani, Faru na diwani wa Mnyamani, uliosema haukuwa na taarifa kutoka Rahco kama watabomoa nyumba hizo.

“Tume iliwasiliana na Uongozi wa Rahco ulisema hilo ni eneo la mradi wa Reli ya Standard Gauge na kwamba hata ramani ya Mnyamani inaonesha eneo hilo lipo ndani ya mita 30 za reli tofauti na madai ya wananchi,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema Tume iliziandikia pande zote mbili barua Machi 7, mwaka huu kuzitaka ziwasilishe vielelezo vyao ifikapo Machi 13, mwaka huu na kuzitaka pande zote mbili kuwasili mbele ya Tume ili zisikilizwe ifikapo Machi 14, mwaka huu.

Alisema baada ya Rahco kupata barua ya Tume ilijibu kuwa haiwezi kuwasilisha vielelezo kwani mwanasheria wao alikuwa safarini ingawa Rahco ilisema utaratibu wa kubomoa nyumba hizo ulifanyika kwa kushirikisha wawakilishi mbalimbali.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com