METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, February 17, 2016

Magufuli arejesha Polisi bandarini


RAIS John Magufuli ameamuru Jeshi la Polisi kurudi bandarini na kufanya kazi za ulinzi wa bandari pamoja na mita za kupimia mafuta.

Tayari Jeshi la Polisi limeshatekeleza agizo hilo la Rais na askari Polisi sasa wanafanya kazi ya ulinzi katika Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine zote nchini.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) miaka ya nyuma iliamua kuwaondoa Polisi bandarini na kuunda kikosi chao cha ulinzi cha Polisi, ambao walikuwa wakisaidia ulinzi bandarini.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alitangaza maamuzi hayo ya Rais jijini Dar es Salaam juzi na kusema huo ni utekelezaji wa kile Rais Magufuli alichokisema mwaka jana wakati akitumbua majipu bandarini.

“Kama wananchi ambavyo watakumbuka, huko nyuma kulikuwa na Kitengo cha Polisi Bandarini ambacho kilikuwa kinasaidia ulinzi bandarini, lakini ikafika mahali ambapo Mamlaka ya Bandari ikafikiri wanaweza kuwa na ulinzi wa kwao, sasa Rais ameamua Polisi warudi bandarini na kufanya kazi za ulinzi kama walivyokuwa wanafanya zamani,” alisema Balozi Sefue.

Balozi Sefue pia alisema polisi watawajibika katika ulinzi wa mita za kupimia mafuta zilizopo bandarini hapo, ambako hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alienda na akamsimamisha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo, Magdalena Chuwa.

“Kule kwenye ‘flow meter’ za kupimia mafuta bandarini, ambako Waziri Mkuu alienda na kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo, zile ‘flow meter’ lazima zilindwe na polisi sasa,” alisema Balozi Sefue.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari jeshi hilo, limeshatekeleza amri hiyo ya Rais na askari wake wapo bandarini, wakifanya ulinzi katika maeneo yote yaliyotajwa.

“Tayari Jeshi la Polisi limeshaanza kazi hiyo ya ulinzi bandarini kama ambavyo Rais ameagiza na kesho (leo) tutalizungumzia suala hilo ni kwa namna gani tumejipanga,” alisema Bulimba.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikwenda Bandari ya Dar es Salaam na kubaini kwamba kwa miaka mitano, kipima mafuta (flow meter) kilikuwa hakifanyi kazi hivyo Serikali kupoteza mapato.

Siku moja baada ya kubainika kwa kashfa hiyo, Waziri Mkuu aliwasimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Chuwa na Meneja wa Kitengo cha Bandari, Bernadina Mwijarubi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com