METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 14, 2017

Mtambo wa maji Ruvu Juu sasa kuzalisha kwa wingi

UJENZI wa laini mpya ya umeme wenye nguvu ya Kilovolti 33 kutoka Chalinze kwenda Mlandizi eneo lenye urefu wa kilomita 45 umekamilika mwishoni mwa wiki.

Kukamilishwa kwa ujenzi huo kutawezesha pampu mpya za mtambo wa maji wa Ruvu Juu kusukuma jumla ya lita milioni 196 za maji safi kwa siku.

Taarifa iliyotolewa ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa) ilisema, Mamlaka hiyo kupitia mkandarasi wake wa WABAG kutoka nchini India akishirikiana na mkandarasi msaidizi, kampuni ya M/S Mollel Electrical ya nchini, ilikuwa na kazi ya kupitisha nyaya za umeme ili ziingie katika eneo la mtambo.

Imesema ili kazi hiyo ifanyike pasipo kuleta madhara, laini maalumu kwa ajili ya umeme mkubwa wa kilovolti 33 inayoendesha mitambo ya maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu ililazimika kuzimwa kwa kuwa laini hiyo mpya inapita chini na juu ya laini hizo.

Imebainisha kuwa, kitaalamu ni hatari kufanya kazi ya kupitisha nyaya za umeme chini au juu ya laini za umeme nyingine kubwa zikiwa na umeme.

Mtambo sasa utahitaji jumla ya 16MVA za umeme ili kusukuma maji safi yanayozalishwa kwa asilimia 100 na kazi iliyobaki hivi sasa ni kuunga laini hiyo mpya katika sub-station ya Chalinze ili pampu zote ziweze kufanya kazi.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Dawasa inalishukuru Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa ushirikiano na ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya umeme ambao imekua ikiutoa ili kukamilisha kazi hiyo.

Aidha, imeweka wazi kuwa, vifaa vyote muhimu kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo viliandaliwa na kuwa kazi hiyo imekamilika na umeme umewashwa.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com