METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 10, 2017

Mgodi kuzawadia wanafunzi bora wa kike kidato 4 Kahama

Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu

KATIKA kuhakikisha Mkoa wa Shinyanga unafanya vema katika matokeo ya mitihani ya kumaliza kidato cha nne kwa wanafunzi wa kike, kampuni ya Acacia kupitia mgodi wake wa dhahabu wa Bulyanhulu umeanza programu ya kuwazadia wanafunzi hao wanapofanya vizuri katika masomo yao.

Zawadi hizo zitakuwa zikitolewa kila mwaka katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani. Kwa mwaka huu imewapatia baiskeli wanafunzi wa kike wanane na walimu walezi wawili katika shule za sekondari za Bugarama na Bulyanhulu waliofanya vizuri katika masomo yao.

Akikabidhi baiskeli hizo juzi, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa mgodi huo, Zuwena Sekondo, alisema baiskeli hizo zitasaidia kuwatia hamasa wanafunzi wa kike hasa wanaosafiri umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, ili waendelee kufanya vema katika mitihani ya shule na ile ya kitaifa.

Aliwataja waliozawadiwa baiskeli hizo katika Sekondari Bulyanhulu ni Irene Jimmy wa kidato cha tatu aliyeshika nafasi ya kwanza katika mitihani wa kidato cha pili mwaka jana, huku Zainabu Kisambale wa kidato cha tatu akifanya vizuri katika mitihani ya kidato cha pili kwa kupata daraja la pili.

Wengine ni Maombi Silvester kwa nidhamu shuleni na Rehema Abdallah wa kidato cha nne aliyeshika nafasi ya 10 katika mitihani ya shule na pia mwaka jana akiwa kidato cha tatu alishika nafasi ya tatu.

Aidha, Sekondo aliendelea kuwataja wanafunzi wa kike walipata baiskeli katika sekondari ya Bugarama kuwa ni Jesca Peter wa kidato cha kwanza anayefanya vizuri katika somo la Kiingereza Rozi Juma Omary kidato cha pili aliyeshika nafasi ya 10 katika mitihani wa kitaifa mwaka jana.

Ofisa Maendeleo huyo aliwataja pia Philomena Achoro kidato cha pili aliwahi kushika nafasi ya kwanza akiwa kidato cha kwanza mwaka jana, Evelyn Silasi kidato cha nne aliwahi kushika nafasi ya sita akiwa kidato cha tatu mwaka jana pamoja na mwalimu wao mlezi, Prisca Mwanantemi.

Hata hivyo aliyataka mashirika ya kiserikali na yale yasiyo ya kiserikali kujitoa katika kumpigania mtoto wa kike katika kupata elimu hali ambayo isaidia mtoto wa kike kujiongoza katika maisha yake ya baadae nakuongeza kuwa kutasaidia kupunguza wimbi la wanawake wasio na elimu.

Kampuni ya Acacia imetoa shuka, sabuni, dawa za meno na mafuta kwa wagonjwa katika kituo cha Afya cha Bugarama na Lunguya, lengo likiwa ni kupambana na wimbi la uchafu katika vituo vya afya.

CREDIT: HABARI LEO
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com