
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa
na ni mke wake, Mary Majaliwa (kushoto), akizungumza na wananchi,
wakati alipokagua kituo cha Afya Kibaoni, katika Wilaya ya Kilombero,
mkoani Morogoro, Septemba 17.2019.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akitembelea wagonjwa, kwenye Kituo cha Afya Kibaoni, kilichopo katika
Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Septemba 17.2019.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa
na Daktari Mkuu wa Kituo cha Afya Kibaoni, Happiness Ndosi (kushoto),
akikagua kituo hicho, kilichopo katika Wilaya ya Kilombero, mkoani
Morogoro, Septemba 17.2019.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi wa Kibaoni, katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Septemba 17.2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kupeleka gari la kubebea wangonjwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni
kilichopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara ili kuwapunguzia wananchi
gharama ya kukodi gari kwa sh. 800,000 pale wagonjwa wao wanapopata
rufaa.
Wananchi wa Mji wa Ifakara
wameiomba Serikali iwasaidie kuwapatia gari la wagonjwa kwani kitua
chao hakina gari na wagonjwa wao wanapopata rufaa ya kwenda hospitali ya
Rufaa ya mkoa wa Morogoro wanalazimika kukodi gari kutoka hospitali ya
Mtakatifu Francis kwa gharama ya sh. 800,000 ambazo baadhi yao
wanashindwa kuzimudi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo (Jumanne, Septemba 17, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa Mji
wa Ifakara katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kituo
cha mabasi cha mji huo. Amesema iwapo fedha za makusanyo ya mapato ya
ndani katika halmashauri husika zingekuwa zinatumika vizuri kusingekuwa
na changamoto kama hizo.
Amesema Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha
huduma za afya kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi hao kuendelea kuwa
na imani na Serikali yao. “Nitampigia simu Waziri Ummy (Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) katika mgao ujao alete
gari la wagonjwa hapa.”
Pia, Waziri Mkuu ameielekeza
Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe katika mgawo wa ujenzi wa hospitali za
wilaya, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ipewe kipaumbele kwa sababu eneo
hilo ni kubwa na lina watu wengi lakini hakuna hospitali ya wilaya hivyo
kusababisha msongamano mkubwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni.
“Nimetembelea mwenyewe kituo
cha Afya cha Kibaoni na nimeshuhudia msongamano wa wagonjwa, mgao wa
pili wa ujenzi wa hospitali za wilaya Mji wa Ifakara lazima upewe
kipaumbele. Suala la huduma za afya ni suala nyeti, hivyo ujenzi wa
hospitali hiyo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.”
Awali, Mganga Mfawidhi wa
Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dkt. Happyness Ndosi alisema kituo cha
Afya cha Kibaoni kinapokea na kuwahudumia wagonjwa wa nje 225 hadi 250
kwa siku na wagonjwa wanaolazwa ni kati ya 50 hadi 80 kwa siku.
Wakinamama wanaojifungulia kituoni hapo ni 400 kwa mwezi.
Akizungumzia kuhusu changamoto
zinazikabili kituo hicho amesema kina upungufu wa watumishi 92, kwani
kina jumla ya watumishi 83 huku mahitaji yakiwa ni watumishi
175, ukosefu wa gari la wagonjwa na pia hakina gari lolote la kutolea
huduma zikiwemo za chanjo, na usambazaji, uchakavu kwa baadhi ya majengo
kama la wagonjwa wa n je.
Pia, kituo kinakabiliwa na
ukosefu wa jengo la kutunzia watoto njiti, watoto wachanga na wale
wanaohitaji uangalizi maalumu baada ya kuzaliwa (neonatal unit), ufinyu
wa chumba cha kujifungulia pamoja na ukosefu wa mashine ya kutolea dawa
za usingizi (anesthesia machine).
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema Serikali haitokuwa na msamaha na watendaji wa halmashauri
watakaobainika kutafuna fedha za makusanyo ya mapato ya ndani pamoja na
fedha zinazotolewa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi mbalimbali
ya maendeleo kwenye maeneo yao.
“Fedha za mapato ya ndani
hazitumiki vizuri watu wanadukua mifumo, wanapaswa watambue kwamba
Serikali ipo makini wakati wote. Watumishi wote watakaobainika
kujihusisha na vitendo hivyo vya ubadhilifu hatua kali za kinidhami
zitachukuliwa dhidi yao. Watumishi wa umma mnatakiwa kutekeleza majukumu
yenu kwa weledi.”
Waziri Mkuu amesema watumishi
wa umma wanatakiwa kujiepusha na migogoro kwa kuwa ni kunyume na
taratibu za kiutumishi. “Haiwezekani viongozi wakagombania zabuni
zitokanazo na fedha za kodi za wananchi, kwa ajili ya maslahi yao
binafsi. Serikali itasimamia zabuni zote.”
0 comments:
Post a Comment