Wajumbe wa mkutano wa Mabadiliko ya
tabia ya nchi na athari zake kiuchumi hapa nchini uliokishirikisha Chuo
cha Mipango ya Maendeleo Vijijini –Dodoma na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya
(EU), wakiingia kwenye ukumbi wa Mikutano mmoja Jijini Dar es salaam,
siku ya kwanza ya mkutano huo wa Siku mbili.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo
cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina (kulia)
akifafanua jambo wakati wa mkutano uliohusu changamoto za mabadiliko ya
tabia ya nchi wakati wa mkutano uliowashirikisha wadau wa maendeleo
kutoka ndani nan je ya nchi na kuandaliwa na Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini-Dodoma.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo
akichangia mada mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi
yanavyoathiri uchumi wa wananchi vijijini nchini Tanzania,
zilizowasilishwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini-Dodoma, na kufanyika Jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wadau wa mkutano uliohusu
changamoto za athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya
nchi wakifuatilia kwa makini mjadala kuhusu suala hilo, Jijini Dar es
Salaam.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo
cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina
(kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Frank Hawassi (kulia) wakiwa katika
picha ya pamoja nje ya ukumbi wa mkutano kuhusu Mabadiliko ya Tania
Nchi uliowashirikisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi uliofanyika
Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo
vijijini – Dodoma Dkt. Frank Hawassi akizungumza na wajumbe wa Taasisi
na Washirika wa Maendeleo kuhusu, umuhimu wa kuunganisha nguvu katika
kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi, katika Mkutano wa Mabadiliko ya
Tabia nchi jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo
cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina
akizungumza na wadau na Washirika wa Maendeleo kuhusu mradi wa Chololo
Ecovillage uliopo Dodoma unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) wakati wa
Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi jijini Dar es salaam.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM).
Na Benny Mwaipaja,WFM
Wadau wanaofanya tafiti mbalimbali za
Maendeleo ya uchumi nchini hasa maeneo ya vijijini kuhusu Mabadiliko ya
Tabia nchi wametakiwa kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo Serikalini na
katika Mashirika mengine ya Maendeleo ili matokeo yake yafanyiwe kazi na
kusudio la tafiti hizo liweze kufikiwa.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam
na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo
vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina wakati wa Mkutano uliohusu
mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kiuchumi uliozihusisha Taasisi
za Serikali na Binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.
Amesema Chuo cha Mipango kimekuwa
kikifanya kazi zake vijijini, zikiwemo za tafiti mbalimbali na matokeo
hayo huwasilishwa katika ngazi husika ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais
inayoshughulikia mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili
kutumia matokeo hayo kwa manufaa ya maendeleo ya jamii hasa vijijini.
“Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi
ambao umejadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za kiuchumi
zinazotokana na Mabadiliko hayo, umetokana na andiko la Wanafunzi wa
Chuo hicho waliokwenda katika mafunzo kwa vitendo vijijini na kushuhudia
namna mabadiliko ya tabia nchi yalivyoathiri maendeleo ya wananchi”.
Alifafanua Prof. Lokina
Tayari Chuo kina mradi ujulikanao kama
Chololo Ecovillage unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) Mkoani Dodoma,
ambao huwafundisha wanakijiji njia bora za uzalishaji mali, hivyo
kuwafanya baadhi ya Wananchi waliokuwa wanakosa chakula, kutokana na
hali ya Ukame wa Mkoa huo kuanza kupata mazao ya kutosha na kuongeza
pato lao.
Naye Mkuu wa Chuo hicho cha Mipango ya
Maendeleo vijijini- Dodoma, Dkt. Frank Hawassi, amezitaka Taasisi na
Mashirika ya umma na Binafsi kuunganisha nguvu katika kukabiliana na
Mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuwa kama juhudi hazitachukuliwa athari
zake zitampata kila mmoja.
Aidha, amesema hakuna nchi inayoweza
kufanikiwa kukabiliana na tatizo hilo bila kushirikiana hata kama nchi
hiyo imeendelea kwa kiasi kikubwa. Pia Jamii inapaswa kujua kuwa hata
matatizo ya wafugaji, wakulima na wengine kuhusu ardhi ni matokeo ya
athari za Mabadiliko ya Tabia nchi, hivyo kila mmoja anatakiwa kuwa
chachu ya utunzaji wa mazingira, ili maendeleo yanayopatikana yawe
endelevu.
Ameongeza kuwa Chuo cha Mipango Dodoma
kinatoa nafasi kwa wadau kote nchini kukitumia kikamilifu katika kutatua
changamoto za kimazingira kwa kuwa ipo Idara iliyo na jukumu la
kushughulikia suala la Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi.
Kwa upande wake aliyekuwa Balozi wa
Umoja wa ulaya nchini Tanzania Tim Clarke, ambaye ameongoza timu ya
washirika wa Maendeleo katika Mkutano huo ameitaka Serikali kupitia
Wizara ya Nishati na Madini kujitahidi kuwahamasisha wananchi kutumia
Nishati mbadala ikiwemo Gesi ili kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu
kwa kukata miti kwa ajili ya kupata Mkaa.
Vilevile ametoa rai kwa Serikali kuwa
karibu na jamii na kuwaelimisha kuhusu kutunza mazingira katika shughuli
zao za kila siku za kujipatia kipato ili kusaidia kulinda mazingira ya
asili yatakayochochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa
ujumla.
0 comments:
Post a Comment