Katibu
Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machura akitoa hotuba ya
kufunga mafunzo ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa
washirika wa maendeleo kwa Mkoa wa kigoma. Kulia ni mmoja wa wakufunzi
wa mafunzo hayo, Dkt. Wilhelm Ngasamiaku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, kushoto ni Mratibu wa mafunzo hayo Bw. Paul Sangawe kutoka Tume
ya Mipango.
Mratibu
wa Mafunzo Bw. Paul Sangawe akitoa muhtasari wa kile kilichojadiliwa
katika mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa siku tano. Katikati ni Katibu
Tawala Msaidizi Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machura na kulia ni mmoja wa
wakufunzi wa mafunzo hayo, Dkt Wilhelm Ngasamiaku kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam.
Mchumi
kutoka Wizara ya Fedha na Mipango – Tume ya Mipango, Bw. Senya Tuni
akionesha kitabu cha Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2016/17-2020/21) kwa washiriki (hawapo pichani) wakati akiwasilisha
mada juu ya Mpango huo.
Baadhi
ya washiriki wakifanya mazoezi ya kanuni zinazotumika kuchagua miradi
sahihi kwa ajili ya kupata ufadhili kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Mazoezi hayo yalifanyika mapema kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki akichangia mada kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki akichangia mada kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
Na Adili Mhina, Kigoma
Serikali
imewaonya watumishi wasio waaminifu katika kusimamia na kuratibu miradi
inayotekelezwa kwa fedha za washirika wa maendeleo kuepukana na vitendo
vya rushwa na ubadhirifu kwani Serikali ya Awamu ya Tano haina huruma
wala msamaha kwa watu wa aina hiyo.
Onyo hilo
limetolewa mwishoni mwa juma na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Kigoma
Bw. Daniel Machura wakati akifunga mafunzo ya maandalizi ya miradi ya
maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa mkoa wa
Kigoma yaliyofanyika mjini hapa na kuendeshwa na Wizara ya Fedha na
Mipango kupitia Tume ya Mipango kwa ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji.
Mafunzo
hayo yalishirikisha Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Makatibu tawala wa wilaya, Wakuu wa Idara za Mipango, Wachumi, Maafisa
Mipango na Watakwimu ambao wana majukumu ya usimamizi na uratibu wa
miradi katika sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma na Halmashauri zake zote.
Machura
alieleza kuwa Serikali ya sasa haina nafasi ya kuwalea watendaji ambao
wanaweka maslahi yao mbele badala ya kuangalia wananchi katika
kutekeleza miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo kitu
kinachopelekea miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango bila kuzingatia
thamani ya fedha.
Alieleza
kuwa baadhi ya watumishi walifikia hatua ya kuandaa maandiko ya kuomba
fedha za ufadhili wa miradi ya maendeleo ya wananchi lakini fedha hizo
zikipatikana walikuwa wanagawana na kuzitumia katika shughuli zao
binafsi badala ya kuzingatia malengo ya fedha hizo.
“Tulifika
pabaya sana, watu walikuwa wanaandika proposal (andiko) kwa wafadhili
ili wapate fedha za kutekeleza miradi ya wananchi lakini cha ajabu
unakuta fedha zikipatikana wanagawana bila aibu kwa kuwa zimetoka nje,
katika serikali ya sasa watu wa aina hiyo hawana nafasi kwenye utumishi
wa umma,” alieleza Bw. Machura.
Alisisitiza
kuwa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa hawana budi kuzingatia
mafunzo waliyopata kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kusimamia miradi
na kuleta maendeleo katika maeneo yao ya utawala ili wafadhili waendelee
kuamini kuwa fedha zote wanazotoa zinatekeleza miradi iliyokusudiwa.
“Tukifanya
hivyo Serikali ya Ubelgiji pamoja na wadau wengine wa maendeleo
watakuwa tayari kuongeza michango yao katika kuusaidia mkoa wetu
kujikomboa kutoka katika umaskini hususan kwa kuendelea kufadhili miradi
mbalimbali ya maendeleo”, alisistiza.
Kwa
upande wake mratibu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji
anayesimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Uchumi Tume
ya Mipango, Bw. Paul Sangawe alibainisha kuwa kuna baadhi ya watendaji
ambao hawatoi taarifa za matumizi ya fedha za miradi ya ufadhili kwa
wakati, kitu ambacho kinarudisha nyuma jitihada za washirika wa
maendeleo katika kufadhili miradi.
Kutokana
na hali hiyo, Sangawe alishauri uongozi wa Ofisi ya Mkoa wa Kigoma
kujiwekea utaratibu wa kukaa na halmashauri zake mara kwa mara ili
kuangalia maendeleo ya miradi inayotekelezwa kwa fedha za washirika wa
maendeleo na kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na malengo
husika.
Aidha,
Sangawe alisisitiza kuwa ni lazima mamlaka zinazohusika katika kufanya
makubaliano ya mikataba na wafadhili kuwa makini na kuzingatia kuwa
miradi inayotaka kufadhiliwa ni ile yenye tija kwa wananchi na ambayo
inaharakisha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2025 ya kuipeleka
Tanzania katika uchumi wa kati.
0 comments:
Post a Comment