Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akitoa
kauli ya Serikali kuhusu utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu
kwa mwaka wa masomo 2016/2017 katika Mkutano wa Tano wa Bunge la 11
unaoendelea mjini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma
Jumla ya
wanafunzi 119,012 wa Elimu ya Juu nchini wametengewa kiasi cha shilingi
bilioni 483 Katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kupewa mikopo
itakayowasaidia kujikimu pindi watakapokuwa vyuoni.
Kiasi
hicho cha fedha kimetajwa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akitoa kauli ya
Serikali kuhusu utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka
wa masomo 2016/2017.
Prof.
Ndalichako amesema kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa kuzingatia malengo ya
Mfuko wa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo kigezo kikuu
kimekuwa ni uhitaji wa mwanafunzi pamoja na fani za kipaumbele anayosoma
mwanafunzi.
Fani za
kipaumbele kwa mujibu wa Wizara hiyo ni pamoja na Sayansi za Tiba na
Afya, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi
Asilia na Mifugo, Uhandisi wa Viwanda pamoja na Kilimo na Umwagiliaji.
Prof.
Ndalichako ameongeza kuwa kuna baadhi ya wanafunzi ambao wamedahiliwa
kwenye fani za kipaumbele lakini hawana vigezo vya kupewa mikopo
kutokana na tathmini ya uhitaji kuonesha kuwa wanaweza kusomeshwa na
wazazi au walezi wao.
“Kwa
mwaka huu wa fedha, Serikali imeongeza kiasi cha fedha zinazotakiwa kwa
ajili ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu waliochaguliwa na
wanaondelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini kutoka shilingi
bilioni 473 hadi bilioni 483 ambayo itaweza kugharamia wanafunzi
wanaoanza 25,717 na wanaoendelea na masomo 93, 295”, alisema Prof.
Ndalichako.
Ameongeza
kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali za utoaji mikopo ambazo pamoja
na mambo mengine zinachangiwa na mfumo wa udahili wa wanafunzi katika
Vyuo vya Elimu ya Juu ambapo kwa sasa kuna mgongano kati ya Tume ya Vyuo
Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu pia kutokuwa na tarehe moja ya Taasisi
zote za Elimu juu ya kufungua vyuo kunaleta mkanganyiko.
Akiongelea
kuhusu wanafunzi wanaoanza chuo mwaka huu, Prof. Ndalichako amesema
kuwa jumla ya wanafunzi 58,010 wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu na
orodha yao tayari ilishawasilishwa katika Bodi ya Mikopo na hadi kufikia
Novemba 2 mwaka huu jumla ya wanafunzi 21,190 wameshapewa fedha hizo.
Waziri
amefafanua idadi ya wanafunzi hao waliopata mikopo kuwa 4,321 ni
yatima,118 wana ulemavu na wanafunzi 87 ni wale waliosoma shule za
Sekondari kwa ufadhili wa watu binafsi au Taasisi mbalimbali.
Aidha,
Prof. Ndalichako amesisitiza kuwa jumla ya wanafunzi 25,717 wanaoendelea
na masomo waliokuwa na mikopo wataendelea kupatiwa mikopo hiyo kama
ilivyokuwa katika mwaka wa masomo uliopita.
“Napenda
kuwatoa hofu wanafunzi wanaoendelea kuwa Serikali haijafuta mkopo kwa
mwanafunzi yoyote anayeendelea na masomo, kwa wanafunzi ambao vyuo vyao
vimewasilisha taarifa za matokeo ya wanafunzi wao Bodi imekwishawatumia
fedha zao za mkopo”, alisema Prof Ndalichako.
0 comments:
Post a Comment