METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, October 3, 2016

Wizara yazindua kondomu kukabili ukimwi

WIZARA ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua kondomu za kiume mpya aina ya Zana na kuzisambaza maeneo ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na za rufaa za mikoa ili zitolewe bila malipo kwa ajili kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na magonjwa yatokanayo na zinaa.

Mganga wa Mkoa wa Morogoro, Dk Frank Jacob , alisema hayo katika hotuba iliyosomwa na Kaimu Mganga wa mkoa huo, Dk Samson Tarimo, wakati wa uzinduzi wa kondomu ya Zana, kwa upande wa mikoa ya Pwani na Morogoro.

Dk Jacob alisema tangu kugundulika kwa Ukimwi nchini mwaka 1983, serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau wengine, imekuwa ikichukua juhudi za makusudi kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Wizara pia imekuwa ikitoa huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na maambukizi ya VVU na katika hatua hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine , imekuwa ikisambaza kiasi kikubwa cha kondomu za kiume.

Dk Jacob alisema utafiti wa viashiria vya Ukimwi na Malaria wa mwaka 2011/2012 kwa Watanzania uliweka bayana kwamba licha ya asilimia 69 ya wanawake na 77 ya wanaume miongoni mwa Watanzania watu wazima, wanafahamu matumizi ya kondomu. Hata hivyo alisema ni asilimia 27 ya watu hao wenye wenza zaidi ya mmoja walitumia kondomu mara ya mwisho walipofanya ngono.

Dk Jacob, alisema baada ya kufanya utafiti na kutafakari kuhusu matumizi duni ya kondomu miongoni mwa Watanzania, Wizara ilibaini kuwa kukosekana kwa utambulisho katika kondomu inayotolewa bila malipo na serikali kumechangia kwa baadhi ya watu kukotumia kondomu.

Hivyo wizara kwa kushirikiana na wadau wengine imeboresha kondomu inayotolewa bila malipo na serikali kuipa jina la Zana ili kuvutia watumiaji na kuongeza kasi ya kudhibiti maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa Watanzania.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa kudhibiti Ukimwi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Shoka Subira , alisema tayari kondomu milioni 21 zimesambazwa nchini kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com