WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Angella Kairuki ameitaja Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuwa
ndio inayoongoza kwa vitendo vya rushwa kisekta nchini, kutokana na
kuwa na majalada mengi ya kesi za rushwa zinazoendelea mahakamani.
Aidha, amebainisha kuwa Mahakama ya Ufisadi iko mbioni kuanza kazi,
baada ya Jaji Mkuu kukamilisha kutengeneza kanuni za uendeshaji pamoja
na mafunzo kwa majaji.
Akizungumza katika kikao kati ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali ya
Mtaa mjini Dodoma jana, Kairuki alisema kwa mujibu wa mchanganuo wa
kesi zilizopo mahakamani kisekta kuanzia Juni mwaka huu, zinaonesha
mamlaka hiyo na sekta ya afya ndio zinaongoza kwa kuhusishwa na vitendo
vya rushwa.
Alisema mchanganuo huo unaonesha kuwa hadi Juni mwaka huu, kesi
zilizopo mahakamani za kisekta ni 509 na kati ya hizo kesi 209 sawa na
asilimia 41 zinaihusu Serikali za Mitaa na kufuatiwa na sekta ya afya
ambayo ina kesi 63 sawa na asilimia 12.
“Sekta hii pia kwa mwaka 2015/16 imeonekana kuongoza kwa kuwa na
majalada mengi yanayohusu tuhuma za rushwa. Kati ya majalada 3,082
yanayoendelea na uchunguzi, majalada 1,357 sawa na asilimia 44 yanahusu
mamlaka hii,” alisisitiza.
Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua katika kuzuia na kupambana
na rushwa katika eneo hilo hilo la mamlaka ya serikali za mitaa
kutokana na kuongoza kwa kuwa na tuhuma na kesi nyingi za rushwa
zinazoendelea mahakamani.
Kuhusu hatua za kuanzishwa kwa Mahakama ya Ufisadi zilipofikia,
Kairuki alisema mahakama hiyo ipo mbioni kuanza kazi na mashauri yake
yatachukua muda wa miezi tisa kusikilizwa na kutolewa maamuzi.
“Jaji Mkuu ameshamaliza kuandaa kanuni na majaji wameshapewa mafunzo
na maelekezo kwamba ndani ya miezi tisa shauri ziwe zimekamilika,”
alisema.
Kuhusu utendaji wa taasisi ya Takukuru, waziri huyo alisema kwa
kipindi cha mwaka 2015/16 kesi mpya 424 zilifunguliwa katika mahakama
mbalimbali nchini ikiwa ni ongezeko la kesi 110 ikilinganishwa na mwaka
2014/15.
Pia alifafanua kuwa kati ya kesi hizo, kesi 177 zilihusu kifungu cha
15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 na kesi 247
zilihusu vifungu vingine, ambavyo mashitaka dhidi ya watuhumiwa
mahakamani yanahitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma na
katika kesi hizo kesi kubwa zilizokuwa 15. Pia alisema Takukuru
imefanikiwa kuokoa Sh 43.78 ikiwa ni ongezeko la Sh 36.78 bilioni
ziliozookolewa mwaka 2014/15.
Alisema fedha hizo zilitokana na kitendo cha taasisi hiyo kuanzisha
kitengo cha ufuatiliaji wa fedha na mali za watuhumiwa zilizopatikana
kwa njia ya rushwa kwa kutaifishwa kwa mali za watuhumiwa.
Kwa upande wa wajumbe wa kamati hiyo walibainisha kuwa adhabu
inayotolewa kwa watu wanaotiwa hatiani kwa vitendo vya rushwa haiendani
na kosa wanalolitenda.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza aliishauri serikali
kuchukua hatua za kudhibiti tatizo la rushwa kwa kuwaboreshea maslahi
watendaji wadogo ili kuondokana na rushwa ndogondogo.
Alisema serikali inatakiwa iweke mikakati ya kudhibiti rushwa kuanzia
ngazi za chini ikiwemo kuingiza somo la rushwa katika mitaala ya shule.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Takukuru,
Alex Mfungo alifafanua kuwa upelelezi wa kesi za rushwa, umekuwa
ukichelewa kwa sababu wanataka kujiridhisha kwanza kabla ya kupeleka kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Tuesday, October 25, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Wafanyakazi wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, wakiwa wamejipanga tayari kwa maandamano katika maadhimisho ya S...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akifurahia jambo pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment