METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 25, 2016

Walimu 4 watumbuliwa tuhuma za mapenzi

WALIMU wanne wa Shule ya Sekondari Kitumbeine wilayani Longido Mkoa wa Arusha, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi baada ya kutuhumiwa kujihusisha na mapenzi na wanafunzi wao.

Akisoma risala kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye yupo wilayani humo kwa ziara ya siku tano ya kukagua maendeleo na changamoto, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisema hivi sasa uchunguzi unafanyika, kubaini jinsi walimu hao walivyojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao.

Chongolo alisema uchunguzi utakapokamilika na ikithibitika, watachukuliwa hatua za kinidhamu. Alisema pia kuwa kuna changamoto ya mimba ya utotoni, ambazo baadhi ya wazazi na walezi wao wamekuwa wakiwaozesha kutokana na mila.

Alisema serikali inafuatilia wazazi wenye tabia hiyo ya kuwaozesha watoto kwenye umri mdogo kwani tatizo hilo lipo kwa asilimia 13 katika jamii ya wafugaji.

Hata hivyo, alisema mimba za utotoni zimepungua kutoka sita mwaka 2013 na kufikia nne ingawa bado kuna changamoto ya wasichana kuozeshwa kwenye umri mdogo na wazazi wao.

"Tupo kwenye uchaguzi ili kubaini kama kweli walimu hao wamehusika na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao au la na endapo ikithibitika kuhusu hilo hatua kali za kinidhamu zinafanyika," alisema bila kuwataja majina wahusika hao.

Aidha, alisema wilaya hiyo pia ina upungufu wa miundombinu ya madarasa 128, nyumba za walimu 281, matundu ya vyoo 393 na madawati 1,320 ambapo katika mwaka huu wa fedha 2016/17 wilaya imejitahidi kujenga madarasa 60, nyumba za walimu saba pamoja na kuongeza shule za msingi sita ili kupunguza tatizo hilo. Baada ya Gambo kupokea taarifa hiyo, alishiriki kupaua bweni la Shule ya Sekondari Longido lililoungua.

Alitoa rai kwa polisi kufanya doria za mara kwa mara shuleni ili kudhibiti matatizo ya moto na kuimarisha usalama wa wanafunzi, pia wanafunzi kushirikiana kwa pamoja na walimu ili kuimarisha ulinzi nyakati za masomo ya usiku.

Alisisitiza kuwa serikali inawasaka wale wote waliohusika na kitendo cha uchomaji moto shule mbalimbali mkoani humo ili kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.

Alitoa rai kwa viongozi wa vijiji, kuhakikisha wanashiriki kupanga ulinzi kwenye maeneo yao ili kudhibiti mambo mbalimbali ya uvunjifu wa amani ikiwemo suala la moto.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com