JOPO la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa nchini, waliokuwa
wakisikiliza kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Longido mkoani Arusha,
wamesema kuwa hawatatoa uamuzi wa kesi hiyo mpaka Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG) na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido, watakapoingizwa
katika rufaa hiyo.
Uamuzi huo umetolewa jana na majaji watatu waliokuwa wakisikiliza
rufaa hiyo, iliyokatwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Onesmo Ole
Nangole.
Majaji hao ni pamoja na Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Sauda Mjasiri,
Jaji Mussa Kipenka na Jaji Profesa Juma Mussa. Katika hukumu hiyo
iliyosomwa jana na Msajili wa Mahakama ya Rufaa nchini, John Kahyoza,
majaji wameungana na hoja ya wakili wa mjibu maombi, Dk Masumbuko Lamwai
aliyesema wahusika hao, walipaswa kuunganishwa katika rufaa hiyo.
Msajili Kahyoza alisema majaji walikubaliana na Dk Lamwai, lakini
hawakukubaliana na hoja ya pili ya aliyotaka rufaa hiyo itupiliwe mbali
kwani ilikosewa kwa kutowaunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido.
Alisema uamuzi wa majaji umesema hauwezi kuitupilia mbali rufaa hiyo
bila ya kuwasikiliza, hivyo imetoa mwanya na nafasi kwa mkata rufaa
kukata rufaa upya na kuwaunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
Msimamizi wa Uchaguzi ndani ya siku 21 ili rufaa hiyo ipangiwe upya
tarehe na kusikilizwa tena.
Msajili alisema jopo la majaji limezingatia vitu vingi sana vya
kisheria na kugundua kuwa rufaa hiyo imekosewa kisheria, kama Dk Lamwai
alivyosema, lakini limeshindwa kuamua kutupilia mbali bila ya
kuwasikiliza na ndio maana imetoa muda wa mkata rufaa kukata rufaa upya
na kuwaingiza wahusika hao kusikiliza hoja zao ili watoe maamuzi.
“Mahakama ya Rufaa kama itatoa uamuzi bila ya kuwasikiliza
Mwanasheria wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi itakuwa imewatia hatia
bila ya kuwasikiliza wakati ni kinyume cha sheria na taratibu za
kimahakama,” alisema na kuongeza:
“Kisheria ni lazima mhusika au wahusika wanapaswa kuwapa nafasi ya
kujitetea mbele ya mahakama hii na hatimaye majaji kutoa uamuzi wa rufaa
bila shaka yoyote.”
Kutokana na hali hiyo, Msajili alisema jopo la majaji watatu limetoa
kibali kwa mkata rufaa, kurekebisha kasoro katika rufaa yake na
kuwaingiza AG na Msimamizi wa Uchaguzi na marekebisho hayo yafanywe
ndani ya muda wa siku 21 na sio vinginevyo.
Baada ya marekebisho hayo, mahakama hiyo itapanga tarehe upya ya kusikiliza rufaa katika mahakama hiyo na kutolea maamuzi.
Wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo wiki iliyopita, mawakili Dk
Lamwai, Edmund Ngemela na Daudi Haraka wanaomtetea mjibu maombi
aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Dk Stephen Kiruswa, waliwaomba
majaji watatu kutupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosekana kuunganishwa
kwa AG na Msimamizi wa Uchaguzi katika rufaa hiyo.
Dk Lamwai alidai mbele ya majaji hao kuwa mleta maombi katika
mahakama hiyo, mawakili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani
Arusha, Onesmo Ole Nangole hawajafanikiwa kuiomba mahakama hiyo kutengua
uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha uliotengua ubunge wake Juni 29,
mwaka huu.
Alidai hukumu ya Jaji Silvangirwa Mwangesi, ilikuwa imezingatia mambo
yote ya msingi na kutengua ubunge huo na wameiomba Mahakama ya Rufaa
kukubaliana na hukumu hiyo bila ya kupingamizi.
Alidai uchaguzi wa Longido, ulipikwa na kuchakachuliwa na hilo
lilionekana katika hukumu ya Jaji Mwangesi na ndio maana alitengua
ubunge huo.
Tuesday, October 25, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Wafanyakazi wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, wakiwa wamejipanga tayari kwa maandamano katika maadhimisho ya S...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akifurahia jambo pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment