Tuesday, October 25, 2016

Hukumu kesi ya Ole Nangole yaahirishwa

JOPO la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa nchini, waliokuwa wakisikiliza kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, wamesema kuwa hawatatoa uamuzi wa kesi hiyo mpaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido, watakapoingizwa katika rufaa hiyo.

Uamuzi huo umetolewa jana na majaji watatu waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo, iliyokatwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Onesmo Ole Nangole.

Majaji hao ni pamoja na Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Sauda Mjasiri, Jaji Mussa Kipenka na Jaji Profesa Juma Mussa. Katika hukumu hiyo iliyosomwa jana na Msajili wa Mahakama ya Rufaa nchini, John Kahyoza, majaji wameungana na hoja ya wakili wa mjibu maombi, Dk Masumbuko Lamwai aliyesema wahusika hao, walipaswa kuunganishwa katika rufaa hiyo.

Msajili Kahyoza alisema majaji walikubaliana na Dk Lamwai, lakini hawakukubaliana na hoja ya pili ya aliyotaka rufaa hiyo itupiliwe mbali kwani ilikosewa kwa kutowaunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido.

Alisema uamuzi wa majaji umesema hauwezi kuitupilia mbali rufaa hiyo bila ya kuwasikiliza, hivyo imetoa mwanya na nafasi kwa mkata rufaa kukata rufaa upya na kuwaunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi ndani ya siku 21 ili rufaa hiyo ipangiwe upya tarehe na kusikilizwa tena.

Msajili alisema jopo la majaji limezingatia vitu vingi sana vya kisheria na kugundua kuwa rufaa hiyo imekosewa kisheria, kama Dk Lamwai alivyosema, lakini limeshindwa kuamua kutupilia mbali bila ya kuwasikiliza na ndio maana imetoa muda wa mkata rufaa kukata rufaa upya na kuwaingiza wahusika hao kusikiliza hoja zao ili watoe maamuzi.

“Mahakama ya Rufaa kama itatoa uamuzi bila ya kuwasikiliza Mwanasheria wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi itakuwa imewatia hatia bila ya kuwasikiliza wakati ni kinyume cha sheria na taratibu za kimahakama,” alisema na kuongeza:

“Kisheria ni lazima mhusika au wahusika wanapaswa kuwapa nafasi ya kujitetea mbele ya mahakama hii na hatimaye majaji kutoa uamuzi wa rufaa bila shaka yoyote.”

Kutokana na hali hiyo, Msajili alisema jopo la majaji watatu limetoa kibali kwa mkata rufaa, kurekebisha kasoro katika rufaa yake na kuwaingiza AG na Msimamizi wa Uchaguzi na marekebisho hayo yafanywe ndani ya muda wa siku 21 na sio vinginevyo.

Baada ya marekebisho hayo, mahakama hiyo itapanga tarehe upya ya kusikiliza rufaa katika mahakama hiyo na kutolea maamuzi.

Wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo wiki iliyopita, mawakili Dk Lamwai, Edmund Ngemela na Daudi Haraka wanaomtetea mjibu maombi aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Dk Stephen Kiruswa, waliwaomba majaji watatu kutupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosekana kuunganishwa kwa AG na Msimamizi wa Uchaguzi katika rufaa hiyo.

Dk Lamwai alidai mbele ya majaji hao kuwa mleta maombi katika mahakama hiyo, mawakili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Onesmo Ole Nangole hawajafanikiwa kuiomba mahakama hiyo kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha uliotengua ubunge wake Juni 29, mwaka huu.

Alidai hukumu ya Jaji Silvangirwa Mwangesi, ilikuwa imezingatia mambo yote ya msingi na kutengua ubunge huo na wameiomba Mahakama ya Rufaa kukubaliana na hukumu hiyo bila ya kupingamizi.

Alidai uchaguzi wa Longido, ulipikwa na kuchakachuliwa na hilo lilionekana katika hukumu ya Jaji Mwangesi na ndio maana alitengua ubunge huo.

No comments:

Post a Comment