Rais wa
zamani wa Israel Shimon Perez ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 93.
Peres ambaye hadithi ya maisha yake iliandamana na kuzaliwa kwa taifa la
kiyahudi alifariki mapema leo katika hospitali mmoja mjini Tel Aviv
Mwanawe
wa kiume Chemi, alithibitisha kifo cha babake kwa wanahabari
waliokusanyika nje ya hospitali ambayo Shimon Peres amekuwa akitibiwa
kwa wiki mbili zilizopita. Hali ya Peres ilizorota kufuatia ugonjwa wa
kiharusi wiki mbili zilizopita, uliosababisha kuvuja damu kwenye ubongo.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitoa taarifa akiomboleza kifo cha
Peres.
Alisema
ataandaa kikao maalum cha Baraza la Mawaziri baadaye leo. Baada ya hapo,
kamati maalum itaandaa mipango ya mazishi ambayo wageni wengi mashuhuri
wa kimataifa na viongozi wa dunia wanatarajia kuhudhuria.
Maafisa
wamesema mwili wa Peres utawekwa katika majengo ya bunge Alhamisi ili
kuwapa fursa wananchi kutoa heshima zao za mwisho. Mazishi yake
yamepangwa Ijumaa katika Mlima Herzl, eneo la makaburi ya kitaifa mjini
Jerusalem.
Wakati
habari za kifo cha Peres zikienea, salamu za rambirambi zilianza
kumiminika kutoka Israel na kote duniani. Rais Barack Obama alimwelezea
Peres kuwa mtu aliyejitolea kwa ajili ya Israel.
Alisema mwangaza
umezimika, lakini matumini aliyouachia ulimwengu yataendelea kuwaka
milele.
Rais wa
zamani Bill Clinton na mgombea wa urais wa Democratic Hillary Clinton
walisema wamempoteza rafiki wa dhati. Marais wa zamani George H Bush na
George W Bush pia walitoa salamu zao za rambirambi. Rais wa Ujerumani
Joachim Gauck alisema Peres aliiongoza Israel kuliko mwanasiasa mwingine
yoyote. Aliihudumia nchi yake katika majukumu tofauti na misingi imara
wakati lilipokuja suala la usalama wa Israel na pia nia thabiti wakati
lilipohusika suala la kuendeleza mchakato wa amani na Wapalestina.
Naye
waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alisema
Peres ndiye aliyetengeneza mahusiano mazuri kati ya Israel na Ujerumani
baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Shimon
Perez ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu mara mbili, ni miongoni mwa
kizazi cha mwisho cha wanasiasa walioshuhudia kuzaliwa kwa taifa jipya
la Israel mnamo mwaka 1948.
Alishinda tuzo ya Nobel kwa pamoja na waziri
mkuu Yitzhak Rabin na aliyekuwa kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat
kutokana na mchango wake katika mazungumzo ya mikataba ya Oslo, ambayo
ilitoa fikira ya kuundwa taifa huru la Palestina.
DW
0 comments:
Post a Comment