METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 12, 2016

SEMINA KUBWA YA KARATE AFRIKA MASHARIKI, KATI NA KUSINI YAANZA JIJINI DAR

Senpai Esther Thomas (kushoto) akipangua chudan tzuki (ngumi ya kifua) wakati semina hiyo ikiendelea.
Anafundisha kwa mifano! Shihan Okuma akishambuliwa na Jerome Sensei kama sehemu ya maelekezo katika semina hiyo

Na Daniel Mbega

SEMINA kubwa ya Shotokan Karate kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini, imeanza leo hii jijini Dar es Salaam ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya mchezo huo nchini Tanzania, inaongozwa na mkufunzi mkuu, Shihan Koichiro Okuma (6th Dan), kutoka makao makuu ya chama cha karate cha Japan Karate Association/World Federation (JKA/WF), Tokyo, Japan.
Semina hiyo – maarufu kama JKA/WF- Tanzania Southern, Central & East African Region Gasshuku – ambayo imeandaliwa na chama cha Japan Karate Association/World Federation-Tanzania (JKA/WF-Tanzania) ni ya nane kufanyika ambapo kwa mwaka huu inashirikisha makarateka 45 kutoka Zimbabwe, Zambia, Uganda, Kenya na wenyeji Tanzania.

Kwa mujibu wa JKA/WF-Tanzania, semina hiyo ya wiki nzima inatarajiwa kufikia tamati Jumamosi.

Makarateka ambao wameanza kushiriki leo hii, kutoka Tanzania ni Jerome Mhagama Sensei, Justine Limwagu, Seberian Dagila, Said O. Kissailo, Lulangalila Lyimma, Athumani Kambi, Mikidadi Kilindo Sensei, Marcus George, Khamis K. Sambuki, Hamis Said Mkumbi, Selemani A. Mkalola, Christopher William, Eliasa Mohammed, Adson Aroko Sensei, Nestory Federicko, Daniel Mbega, Willy Ringo Rwezaura Sensei, na Shihan Dudley Mawala Sensei, ambaye alikuwa mgeni mwalikwa.

Makarateka wengine na nchi zao kwenya mabano ni Gibson Sangweni (Zimbabwe), Robert Chisanga (Zambia), Thobias B. Rudhal (Kenya), George Otieno (Kenya), Joshua Oude (Kenya), George Warambo (Kenya), George Okeyo (Kenya), Florence Kieti (Kenya), Asana Mahmoud Ulwona (Uganda), Ofubo Issa Yahaya (Uganda), Magezi Yasiin (Uganda), Wanyika Abdurahman (Uganda), Frederic Kilcher (Ufaransa) na Koichiro Okuma (Japan).

Mkufunzi mkuu wa JKA/WF-Tanzania, Jerome George Mhagama Sensei (5th Dan), amesema hata hivyo kwamba, tofauti na miaka iliyotangulia, safari hii hakutakuwa na mashindano ili kutoa fursa kubwa kwa Shihan Okuma kufundisha vyema na kuwapandisha madaraja makarateka mbalimbali kuanzia ngazi ya Sho-Dan, Ni-Dan, San-Dan na Yon-Dan (1st – 4th Dan).

“Tunataka tupate muda wa kutosha wa kufanya semina pamoja na mitihani, kwani mbali ya kuwapandisha madaraja makarateka mbalimbali, lakini pia kuna ambao watafanya mitihani ya ukufunzi na uamuzi wa kimataifa ili kupanua wigo na kupata walimu na waamuzi wa kutosha katika kanda yetu,” amesema Jerome Sensei, ambaye alipanda daraja Jumanne, Septemba 6, 2016 baada ya kufanya vizuri na kufaulu mtihani wa 5th Dan jijini Nairobi, Kenya chini ya Shihan Okuma.

Hata hivyo, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kesho ambapo makarateka kutoka Zanzibar nao watahudhuria baada ya kushindwa leo kutokana na sababu mbalimbali.

Jerome Sensei amesema kwamba, changamoto kubwa ambayo inawakabili wao pamoja na mchezo mzima wa Karate nchini Tanzania ni kuwekwa pembeni na wadau mbalimbali wa michezo ikilinganishwa na michezo mingine, hali ambayo imekuwa vigumu kwao kupata udhamini.

Ameiomba Serikali na wadau wengine kuutupia macho mchezo huo, kwani unailetea sifa kubwa Tanzania kutokana na mafanikio ya mchezaji mmoja mmoja.

Katika kipindi cha miaka takriban 10, Tanzania imekuwa kinara wa mchezo wa Karate katika kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini ukitoa Afrika Kusini pekee, hatua ambayo imechangiwa na mafanikio binafsi ya Jerome Sensei, ambaye kwa jitihada zake ameshiriki mashindano ya dunia ya Karate mwaka 2012 na kurudia raundi ya nne, mashindano ambayo yalifanyika Pataya, Thailand, ambapo alitolewa na mtu ambaye alikuja kuwa bingwa wa dunia.

Mbali ya hivyo, ameshiriki mashindano mengine jijini Tokyo, Japan lakini pamoja na kutotwaa ubingwa, ameweza kupanda madaraja kwa viwango vya kimataifa na sasa ni mkufunzi, mtahini na mwamuzi wa kimataifa, ambapo ameweka rekodi ya pekee kwa kuwa mkufunzi mwenye umri mdogo kabisa katika historia ya JKA/WF tangu chama hicho kilipoanzishwa Mei 1947.

Kwa mujibu wa rekodi za JKA/WF, Jerome Sensei (36) ni karateka wa pili wa Afrika Mashariki kuwa na hadhi ya Dan Tano (5th Dan) baada ya David Mulwa Sensei wa Kenya, hivyo ameteuliwa kuwa mkufunzi mwenza mkuu wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Shihan Okuma, ambaye ametokea Kenya ambako kulikuwa na semina wiki iliyopita, amesema kuwa ujio wake siyo wa bahati mbaya bali umetokana na jitihada ambazo Tanzania imekuwa ikionyesha katika maendeleo ya Karate, hususan mafanikio yasiyo na kifani ya Jerome Sensei.

“Nimetumwa na makao makuu kuja kuiunga mkono Tanzania pamoja na kufundisha semina hii, najua semina kama hii mara nyingi huwa inafanyika makao makuu tu au katika kanda maalum, lakini kwa vile Tanzania imeonyesha mafanikio makubwa, hatuna budi kuja hapa ili kuwapa fursa makarateka wengi waweze kushiriki.

“Kuja Japan ni gharama kubwa, wengi hawawezi kumudu pamoja na kuwa na nia na mchezo huu, ni wachache tu ambao wanapata bahati ya kuja kuhudhuria, lakini hapa nimefurahi kuona kuna makarateka wengi wana viwango vya juu kabisa na hii ni faraja kubwa kwangu na kwa JKA/WF,” amesema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com