Kansela
wa Ujeruamni Angela Merkel amesema Ujerumani inahitaji suluhisho
madhubuti kuwajumuisha wakimbizi katika soko la ajira la Ujerumani kama
nguvu kazi. Merkel aliyasema hayo baada ya kukutana na kampuni
mbalimbali.
Katika
juhudi za kuyatetea maisha yake katika siasa, Bi Merkel aliwaita wakuu
wa baadhi ya kampuni kubwa kabisa za Ujerumani kwa ajili ya mkutano
mjini Frankfurt kufafanua kwa nini hawajachukua hatua kuwapa ajira
wakimbizi na pia kubadilishana mawazo kuhusu jinsi wanavyoweza
kushirikiana.
Kampuni
nyingi zinahoji kwamba ukosefu wa ujuzi wa lugha ya Kijerumani,
wakimbizi wengi kushindwa kuthibitisha wana sifa au vigezo na pia
kukosekana uhakika wa wao kuendelee kuishi Ujerumani, ina maana hakuna
mengi ambayo kampuni hizo zinaweza kuyafanya katika kipindi kifupi.
Kansela
Merkel ameiambia radio ya rbb-inforadio kwamba ikihitajika, mazingira
maalumu yanaweza yakaandaliwa kuharakisha mchakato wa kuwajumuisha
wakimbizi katika soko la ajira, lakini akakiri hilo pia litachukua muda.
Utafiti
uliofanywa na shirika la habari la Reuters kwa kampuni 30
zinazowakilishwa katika soko la hisa la Ujerumani, DAX, wiki iliyopita,
umebaini kuwa ziliwaajiri jumla ya wakimbizi 63. Hamsini kati yao
wameajiriwa na kampuni ya Deutsche Post DHL, ambayo imesema iliwapa
ajira wakimbizi kupanga na kusambaza barua na vifurushi. Mkuu wa kampuni
ya DHL, Frank Appel, alisema jana kuwa kampuni hiyo sasa imewaajiri
wakimbizi zaidi, hadi kufikia jumla ya 102.
Mkimbizi Hamza Ahmed katika kampuni ya Reuther STC GmbH mjini Fürstenwalde, Ujerumani
Mkurugenzi
wa kampuni ya viwanda ya Ujerumani ya Thyssenkrupp, Heinrich Hiesinger,
alidokeza mapema mwezi huu kwamba kuwaajiri wakimbizi sio suluhisho la
uhaba wa ujuzi na nguvu kazi nchini.
Kampuni
nyingi za Ujerumani, hasa za uzalishaji bidhaa, hupendelea kuwaajiri
wafanyakazi kupitia mipango ya kuwafunza kazi iliyoratibiwa, ambapo
huwafunza vijana kwa muda wa hadi miaka minne kwa ajira zinazohitaji
ujuzi wa hali ya juu, na wakati mwingine kazi maalumu za kampuni. Lakini
kampuni zinasema wakimbizi wengi waliowasili kutoka Syria, Iraq,
Afghanistan na kwingineko, kwa kiwango kikubwa hawajajiandaa kwa mafunzo
ya aina hiyo.
Vurugu eneo la Mashariki
Wakati
haya yakiarifiwa polisi wamevunja makabiliano makali kati ya wajerumani
wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia na wahamiaji wanaotafuta vibali
usiku wa kuamkia leo katika mji wa mashariki wa Bautzen.
Msemaji
wa polisi Thomas Knaup, amesema wanaume na wanawake 80 na wahamiaji
wapatao 20 walikabiliana katika uwanja ulio katikati ya mji huo jana
usiku. Knaup aidha amesema baadhi ya wahamiaji waliwarushia chupa na
vitu vingine maafisa wa polisi ambao waliwakabili kwa virungu na kuweka
uzio kuyatenganisha makundi hayo mawili. Tukio hilo linaashiria ongezeko
la hali ya wasiwasi nchini Ujerumani kuhusiana na sera ya wakimbizi ya
kansela Merkel.
Machafuko ya mjini Bautzen
Mkazi
mmoja mwenye umri wa miaka 18 alihitaji matibabu hospitalini kufuatia
majeruhi ya kukatwa usoni aliyoyapata, polisi wamesema. Wakati gari ya
kubebea wagonjwa ilipowasili katika eneo la tukio, ilishambuliwa kwa
mawe na watu wenye misimamo mikali. Ilibidi gari la pili liagizwe ili
raia huyo wa Morocco apelekwe hospitali.
Mji wa
Bautzen umekabiliwa na maandamano ya Wajerumani wenye misimamo mikali
dhidi ya wakimbizi katika miezi ya hivi karibuni. Mwezi Februari watu wa
kundi lenye msimamo mkali walishangilia wakati makazi ya wakimbizi
yalipokuwa yakiungua katika mji huo na kuwazuia maafisa wa zima moto
kuuzima moto huo.
Upinzani
wa sera ya kansela Merkel ya kuwakaribisha wakimbizi umefikia kiwango
cha juu kabisa Ujerumani, ambayo iliwachukua wahamiaji wapatao milioni
1.1 mwaka 2015.
DW
DW
0 comments:
Post a Comment