METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, September 11, 2016

Kilimanjaro Queens yatakiwa kuleta taji

SERIKALI imewataka wachezaji wa timu ya wanawake ya Kilimanjaro Queens wanaokwenda kushiriki mashindano ya Kombe la Chalenji nchini Uganda kutokuwa wasindikizaji katika mashindano hayo bali kuhakikisha wanarudi na ushindi, kwani wao ndio wanashika nafasi ya kwanza kwa timu za wanawake katika nchi za Afrika Mashariki.

Mashindano hayo yanatarajia kuanza kesho hadi Septemba 20 katika mji wa Jinja nchini Uganda.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu ofisini kwake mjini hapa jana, alipowaaga wachezaji hao waliokuwa njia moja kwenda Uganda baada ya kucheza mechi ya kirafiki na timu ya wanawake ya Burundi.

Kilimanjaro Stars ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Burundi katika mchezo wa kujipima kabla ya kuanza kwa mashindano ya Afrika Mashariki nchini Uganda.

“Michezo ni afya,ni burudani pia soka inapendwa na kila mtu duniani,kumbuka kuwa mnaenda katika nchi ya watu yenye kuwa na tamaduni zake msiende kuwa wasindikizaji,onesheni nidhamu,choteni yale na kujifunza yanayofaa yasiyofaa yaache huko ili mkaendelee kuileta nchi yetu sifa nzuri,”alisema Kijuu.

Alisema mashindano hayo ni njia mojawapo ya kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa hiyo kwa kutumia nafasi hiyo wajifunze yale yatakayoleta tija kwa Taifa letu.
Kwa upande wa nahodha wa timu hiyo, Sophia Mwasikili alisema kuwa wanaahidi kurudi na ushindi mnono kinachohitajika ni Watanzania kuendelea kuwaombea.

Naye kocha Sebastian Nkoma alisema pamoja na timu yake kufanya vizuri, lakini bado yapo makosa madogo madogo ambayo atayafanyia kazi ndani ya muda mfupi uliobaki na ana imani na timu yao. Michuano hiyo itashirikisha mataifa saba, ambao ni wanachama wa Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com