METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, September 11, 2016

Wadau changamkieni netiboli mpate ajira

MCHEZO wa netiboli ni miongoni mwa michezo yenye mashabiki wengi tangu miaka ya sabini na ulichangiwa na timu zenye upinzani mkali kama Jeshi Stars, Bora, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), na zile za Mashirika ya Biashara ya Mikoa (RTC).

Pia ushabiki huo ulikolezwa na kuwepo kwa timu nyingi za ngazi ya wilaya na mikoa zenye majina makubwa na madogo ambazo zilileta ushindani na kuibua hamasa kati ya wachezaji na viongozi wa timu hizo. Hamasa ya michezo ilichangiwa na kuwepo mashirika mengi ya umma, sera ya michezo sehemu za kazi iliyolenga kuwajenga wafanyakazi kiafya kuchochea kukua kwa michezo, ukiwemo wa netiboli kupanda chati nchini na nje ya nchi miaka hiyo ya nyuma.

Kwa mantiki hiyo, tangu zamani michezo ilikuwa sehemu ya kuzalisha ajira, ukiwemo wa netiboli kwa wasichana waliokuwa wanamaliza elimu ya msingi na sekondari wengi waliajiriwa katika mashirika hayo ama idara za serikali na sekta binafsi. Wachezaji wengi mahiri katika mchezo huo walinufaika kuingizwa kwenye ajira katika Taasisi za Serikali hususani kwenye majeshi ya ulinzi na usalama na kwa kiwango kidogo timu za mashirika ya umma na binafsi.

Licha ya mafanikio hayo, changamoto mbalimbali ziliikumba katika sekta ya michezo kufuatia mageuzi ya aina mbalimbali, yakiwemo ya kisera hususani serikali kujiondoa kutoka mfumo wa uendeshaji wa mashirika ya umma na ubinafsishaji. Changamoto hizo ziliendelea kuzorotesha sekta ya michezo baada ya huko nyuma serikali kupitia Wizara ya Elimu kufuta michezo shuleni, hali iliyochangia pia michezo mingi kudorora ukiwemo wa netiboli kutokana na kukosekana kwa vipaji vipya ambavyo vilipaswa kuendelezwa.

Katika kipindi cha mpito, sehemu pekee iliyokuwa ikiendeleza michezo ya aina mbalimbali ni kwenye majeshi ambayo kila mwaka waliboresha timu zao mbalimbali, ikiwa na kushiriki mashindano ya timu za majeshi na mengineyo makubwa ukiwemo mchezo wa netiboli. Mbali na majeshi kuendeleza michezo nchini miaka ya karibuni pia michezo ya aina mbalimbali imeendelezwa na kukuzwa kupitia mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), netiboli ni miongoni mwa michezo inayoshirikishwa.

Kutokana na kukosekana kwa vipaji vipya ambavyo chimbuko lake ni michezo ya shule za msingi na sekondari, Serikali ya awamu ya nne iliamua kurudishwa tena michezo shuleni. Hatua hiyo ilivipa nguvu vyama vya michezo ngazi za wilaya, mikoa na Taifa kuamua kujipanga ili kuendeleza michezo kwa ajili ya kukuza vipaji na kuibuliwa vingine vipya kwa manufaa ya klabu na taifa kwa ujumla.

Kurejeshwa kwa michezo shuleni pia kuliwezesha kuanza kuibuliwa kwa wachezaji vijana wenye uwezo wa kucheza michezo ya aina mbalimbali ukiwemo wa netiboli, hali iliyorejesha matumaini ya kukua kwa michezo nchini. Kuwepo kwa wachezaji wengi wenye vipaji waliosajiliwa na timu mbalimbali, kumetoa fursa ya vyama vya mchezo huo ngazi mbalimbali kuendesha mashindano, ikiwemo ligi daraja la pili na kwanza nchini.

Pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuendeleza michezo nchini, bado netiboli haijapewa msukumo na wadau kuona ni sehemu ya mchezo unaoweza kuwapatia ajira watoto wa kike kama ilivyo mpira wa miguu. Ukweli huo umejidhihirisha katika mashindano ya ligi daraja la kwanza yaliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro ambapo timu 11 kati ya 24 zilizopo katika mikoa 20 ya Tanzania bara ndizo zilizoshiriki.

Makamu Mwenyekiti wa Chaneta Zainabu Mbiro anaeleza katika risala ya chama hicho kuwa ni timu 11 pekee zilishiriki kati ya timu 24 kutoka mikoa 20 ya Tanzania Bara . Anasema, bajeti ya Chaneta ililenga kupata Sh milioni 18 ambazo zingetumika katika uendeshaji wa mashindano hayo lakini ushiriki ndogo wa timu zilizodhibitisha na kulipa ada kuliwezesha kupatikana Sh milioni 4.1 na hivyo kuleta changamoto kadhaa katika uendeshaji wa mashindano hayo.

“Chaneta haina ufadhili, pia timu mbalimbali zilikosa ufadhili, ukata wa fedha, kutopata ruhusa za wachezaji kutoka sehemu zao za kazi kumechangia timu nyingi kushindwa kushiriki ligi ya mwaka huu,” anasema Mbiro.

“Ni wadau wachache wastani wa mmoja ama wawili ndiyo wamejitokeza kutoa msaada wa maji ya kunywa, tunawashukuru wafadhili hawa wachache waliochangia kutoa huduma za maji na kuendelea kuomba wengine wajitokeza ili kuinua mchezo wa netiboli nchini,” anasisitiza Mbiro.

Pia anashauri Serikali kupitia Wizara husika kusimamia michezo ya aina mbalimbali ili ifundishwe shuleni kuanzia kwa wanafunzi wa elimu ya msingi hadi Sekondari kwa kuwa michezo ni sehemu ya ajira ya kujiajiri ama kuajiriwa katika Taasisi za Serikali, Taasisi za Umma, sekta binafsi pamoja na timu za mitaani. Wakati viongozi wa Chaneta ukiendelea kutoa kilio, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, inasema itatafuta namna ya kupunguza changamoto zilizopo katika mchezo huo ili kuwavutia vijana wa kike kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kukuza ajira nchini.

Waziri mwenye dhamana hiyo, Nape Nnauye anaeleza hayo kwenye hotuba yake ya kufunga michuano ya ligi daraja la kwanza ambayo ilisomwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Anastazia Wambura. Pamoja na Serikali kuendelea kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto za mchezo huo, Waziri Nape anawaagiza maofisa wa michezo wa mikoa ambayo timu zao hazikushiriki ligi hiyo kueleza kwa maandishi sababu za kushindwa kwao kushiriki.

“ Nimesikitishwa na uchache wa timu usioridhisha katika mashindano haya makubwa ambao umechangia kuwakosesha wasichana fursa ya kuibua vipaji vyao kupitia michezo hasa wa netiboli,” anasema Waziri Nape kupitia hotuba hiyo. “Serikali haitakaa kimya itatafuta namna ya kupunguza changamoto zilizopo kwenye mchezo wa netiboli ili uweze kuchangia kutoa fursa pana ya ajira kwa watoto wakike,” anasisitiza Nape.

Naye mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, anamsifu Mwenyekiti wa Chaneta, Anna Kibira kwa moyo wa uzalendo katika kuhamasisha mchezo huo nchini na kufanikisha ligi daraja la kwanza. Dk Kebwe anasema mwenyekiti huyo uongozi mzima wa Chaneta umekuwa mstari wa mbele katika kusimamia vyema mchezo huo licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa fedha na ufadhili wa uhakika wa kuendeleza mchezo huo unaopendwa na wengi nchini.

“Nafurahi kukuona Mwenyekiti wa Chaneta Taifa mama Anna Kibira, umedhihirisha kuwa netiboli ipo kwenye damu yako,” anasema Dk Kebwe. “ ...Ndiyo maana pamoja na kushauriwa kupumzika , umeona utumie fursa hiyo kuja kuungana na wachezaji wa timu mbalimbali za Netiboli kwnye mashindano haya mkoani Morogoro na hii umeonesha uzalendo mkubwa na nitawasiliana na Waziri wa sekta hii mheshimiwa Nape ili mchezo huu upingiwe debe,” anasema Dk Kebwe.

Awali, Kibira alimshukuru Mungu kwa kuombewa apone haraka na familia ya wanamichezo nchini wakiwemo wa netiboli na kumwezesha kuhudhuria mashindayo ya ligi daraja la kwanza.

“Nimefarijika kuona wanafamilia wameniombea nipone haraka na nina mshukuru Mungu kwa sala zao na leo hii nipo hapa Morogoro kushuhudia mashindano haya, nimejiona nimepona kabisa,” anasema Kibira.

Katika ligi ya daraja la kwanza Netiboli, Uhamiaji ilitetea taji lake kwa kujinyakulia pointi 20, na kuungana na timu nyingine tano kushiriki ligi ya Muungano. Timu hizo ni Polisi Morogoro iliyomaliza ya pili kwa kufikisha pointi 18, Jeshi Stars nafasi ya tatu kwa pointi 14 na Madini ya Arusha iliyomaliza ya nne kwa kujikusanyia pointi 13, Tumbaku Morogoro ilishika nafasi ya tano baada ya kumaliza kwa kupata pointi 12, wakati timu ya Polisi Arusha ikishika nafasi ya sita kwa kuwa pointi 10.

Timu nyingine zilizoshiriki katika ligi daraja la kwanza mwaka huu na pointi zao katika mabao ni Arusha Jiji (9), CMTU (8), Tanga Jiji (4), RAS Kagera (2) na timu ya Kinondoni kuambulia sifuri.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com