SERIKALI imewataka wachezaji wa timu ya wanawake ya Kilimanjaro
Queens wanaokwenda kushiriki mashindano ya Kombe la Chalenji nchini
Uganda kutokuwa wasindikizaji katika mashindano hayo bali kuhakikisha
wanarudi na ushindi, kwani wao ndio wanashika nafasi ya kwanza kwa timu
za wanawake katika nchi za Afrika Mashariki.
Mashindano hayo yanatarajia kuanza kesho hadi Septemba 20 katika mji wa Jinja nchini Uganda.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu
Salum Kijuu ofisini kwake mjini hapa jana, alipowaaga wachezaji hao
waliokuwa njia moja kwenda Uganda baada ya kucheza mechi ya kirafiki na
timu ya wanawake ya Burundi.
Kilimanjaro Stars ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Burundi katika mchezo
wa kujipima kabla ya kuanza kwa mashindano ya Afrika Mashariki nchini
Uganda.
“Michezo ni afya,ni burudani pia soka inapendwa na kila mtu
duniani,kumbuka kuwa mnaenda katika nchi ya watu yenye kuwa na tamaduni
zake msiende kuwa wasindikizaji,onesheni nidhamu,choteni yale na
kujifunza yanayofaa yasiyofaa yaache huko ili mkaendelee kuileta nchi
yetu sifa nzuri,”alisema Kijuu.
Alisema mashindano hayo ni njia mojawapo ya kuimarisha na kudumisha
ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa hiyo kwa kutumia nafasi
hiyo wajifunze yale yatakayoleta tija kwa Taifa letu.
Kwa upande wa nahodha wa timu hiyo, Sophia Mwasikili alisema kuwa
wanaahidi kurudi na ushindi mnono kinachohitajika ni Watanzania
kuendelea kuwaombea.
Naye kocha Sebastian Nkoma alisema pamoja na timu yake kufanya
vizuri, lakini bado yapo makosa madogo madogo ambayo atayafanyia kazi
ndani ya muda mfupi uliobaki na ana imani na timu yao. Michuano hiyo
itashirikisha mataifa saba, ambao ni wanachama wa Baraza la Soka la
Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
No comments:
Post a Comment