Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anakatishwa tamaa na
viongozi wengi duniani ambao hujali zaidi kusalia madarakani badala ya
kuboresha maisha ya watu wao.
Akikaribia
kuhitimisha miaka 10 ya utawala wake katika Umoja wa Mataifa, Ban
amezungumzia waziwazi hali ya kidunia, mafanikio, kushindwa kwake na
kukatishwa tamaa kama mkuu wa taasisi hiyo katika mahojiano aliyoyafanya
na shirika la habari la Associated Press. Miongoni mwa mambo
aliyoyagusia ni suala la haki za binadamu ambalo amekuwa akilalamikiwa
kwamba hajafanya ya kutosha katika kulizungumzia. Amenukuliwa akisema
kwamba "nina matumaini kwamba katika kipindi cha mrithi wangu, nchi
wanachama watakuwa na umoja zaidi na kuonyesha mshikamano juu ya haki za
binadamu na masuala ya kibinadamu na kwa dhamira yetu tutaweza
kukomesha vurugu kwa kasi zaidi."
Kiongozi
huyo pia amekosoa namna Umoja wa Mataifa unavyofanya kazi akisema ni
suala lisilowezekana kwa katibu mkuu yoyote "kuwa mtu kamilifu"
kwasababu yeye amekuwa mtekelezaji wa maamuzi yanayopitishwa na mhimili
wa taasisi hiyo. Anasema Umoja wa Mataifa ungekuwa na ufanisi zaidi kama
kungekuwepo na mchakato wa kufanya maamuzi na siyo ule unaoihitaji
maafikiano kwa masuala mengi mbele ya Baraza la Usalama na tamko kutoka
katika baraza hilo.
Anasema
suala hili uipatia nguvu nchi moja kuzuia kitu ambacho mataifa yote
wamekubaliana, akiuliza kwamba Je hii ni sawa? katika karne ya 21 ambapo
una mataifa 193 wanachama? alisema Ban.
Mtazamo wake dhidi ya ule wa magharibi
Akilinganisha
mtazamo wake na viongozi wa kimagharibi, Ban amesema mara nyingi
wamekuwa wakizungumza kupitia matamko, ambalo ni jambo jepesi na wakati
mwingine wamekuwa wakimshinikiza kutozungumza au kutembelea nchi. Lakini
anasema alifanya vile alivyotaka kwasababu anaamini mikutano ya ana kwa
ana na viongozi wa dunia ni muhimu katika kupata uungwaji mkono wao wa
kumaliza migogoro au masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi na
kutokemeza umaskini.
Kwa
viongozi wengi, cha muhimu ni kuchaguliwa kwa njia yoyote na
wakishachaguliwa wanatawala watu na wengi hupotoshwa na hawaheshimu
sauti za wananchi. Kuhusu Syria Ban anasema hajui kwanini wameshindwa
kumaliza mgogoro huo. Masuala mengine aliyoyagusia ni pamoja na vitendo
vya udhalilishaji ngono vinavyofanywa na walinda amani dhidi ya wanawake
na wasichana.
Baada ya
kumaliza uongozi wake katibu mkuu huyo atarejea nchini mwake Korea
Kusini " nitajaribu kuona kitu gani ni bora naweza kuchangia katika
maendeleo ya nchi yangu kama katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa"
amesema kiongozi huyo.
Ban Ki
Moon aliyemrithi Koffi Annan 2007 atamaliza uongozi wake mwezi Disemba
na katika kipindi chake atakumbukwa kwa jitihada zake za kupigania
masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, malengo mapya 17 endelevu ya Umoja
wa Mataifa, kuhamasisha usawa wa kijinsia ambapo alifanikiwa kuanzisha
chombo maalumu cha Umoja huo cha kuyashughulikia masuala ya wanawake.
DW
No comments:
Post a Comment