Mkuu wa
Huduma za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo, Raun Swanepoel akizungumza
na waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusu kampuni hiyo kugawa faida
kwa watumiaji wake wa huduma kwa njia ya simu ambapo ni kiasi cha
bilioni 5.6 kwa watumiaji wa Tigo pesa,kushoto kwake ni Meneja chapa
,William Mpinga katika mkutano uliofanyika mwishoni wa wiki iliyopita.
Kampuni
inayoongoza kwa mtindo wa maisha ya kidijitali, Tigo imetangaza tena
gawio la robo mwaka la shilingi bilioni 5.6 kwa watumiaji wa Tigo Pesa
ikiwa ni mara ya tisa kwa kampuni hiyo ya simu kugawa faida hiyo kwa
watumiaji wake wa huduma ya fedha kwa njia ya simu.
Akizungumza
katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa
Huduma za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo, Raun Swanepoel alisema kwa
ujumla kampuni hiyo imeshalipa watumiaji wake wa huduma za fedha kwa
njia ya simu jumla ya shilingi bilioni 46.2 ikiwa ni malipo ya robo
mwaka tangu kuzinduliwa kwa huduma hiyo Julai 2014.
Swanepoel
alisema kwamba katika robo ya pili ya mwaka huu kiwango cha faida
kilipanda na kufikia asilimia 8 kulikosababishwa na kuongezeka kwa
kiwango cha hisa katika mabenki mbalimbali ya biashara.
“Faida
hii ya hisa inalipwa wateja binafsi, mawakala wa reja reja na
washirika wengine wa kibiashara wa Tigo ambao kila mmoja anapokea malipo
yake kulingana na thamani ya fedha zilizowekwa kielektroniki ndani ya
pochi zao za Tigo Pesa,” alisema Swanepoel.
Swanepoel
aliongeza: “Kusema kweli tunafurahi kutangaza ongezeko hili la faida
katika gawio la mara ya tisa mfululizo. Hii inaonesha jinsi
tulivyojikita katika kuwawezesha wateja wetu kufikia huduma za kifedha
pamoja na nchi zima kwa ujumla kupitia huduma za Tigo Pesa”.
Alibainisha
ongezeko la faida la Tigo, kuboreshwa kwa mazingira ya soko na
kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa Tigo Pesa kama moja ya kichocheo
kilichosababisha kuongezeka kwa faida hususani kwa upande wa
wafanyabiashara. Tigo Pesa hivi sasa ina mtandao mkubwa wa
wafanyabiashara zaidi ya 50,000.
Swanepoel
alisema kuwa kama ilivyokuwa hapo awali gawio kwa wateja
linakokotolewa kwa kuangalia wastani wa salio la kila siku la mteja la
Tigo Pesa katika pochi yake ya simu na kuongeza kuwa mpango huu wa
kugawa faida umeainishwa katika kanuni za Benki Kuu iliyotolewa February
2014.
0 comments:
Post a Comment