
- Yaahidi kufanya mabadiliko makubwa ya kisera na kisheria
- Miongoni mwa Sheria zitakazohusika ni Sheria ya Ndoa na Sheria ya Urithi
- Ni katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu - SDG’s
Tanzania
imeahidi kuchukua hatua tano muhimu za kutetetea na kuendelea haki za
wanawake kati ya sasa na mwaka 2030, ikiwa ni pamoja na kufanya
mabadiliko makubwa ya kufuta sheria zinazokandamiza wanawake na kutunga
sheria za kuleta usawa wa kijinsia, yote katika utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo Endelevu (SDG) mapya kwa manufaa ya wanawake wa Tanzania.
Miongoni
mwa hatua hizo itakuwa ni pamoja na kufuta ama kufanya mabadiliko ambayo
yanaendeleza vitendo vya kiutamaduni ambavyo kwavyo vinaendeleza
ubaguzi wa wanawake kama vile Sheria ya Ndoa, Sheria ya Urithi na
kutunga Sheria ya Kukomesha Ukatili dhidi ya wanawake.
Msimamo
huo wa Tanzania umeelezwa Jumapili, Septemba 27, 2015 na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipozungumza
katika Mkutano wa Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Akinamama: Dhamira
ya Kuchukua Hatua uliohudhuriwa na wakuu wa nchi mbali mbali duniani
kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani.
Rais
Kikwete ameuambia mkutano huo ulioitishwa kwa pamoja na Jamhuri ya Watu
wa China, Denmark, Mexico na Kenya kuwa hatua ya pili ambayo Tanzania
inakusudia kuchukua ni kuridhia makubaliano yote ya kimataifa kuhusu
haki za akinamama hasa Makubaliano ya Kimataifa Juu ya Kukomesha Aina
Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake – Convention on the Elimination of All
Forms of Discrimination Against Women (CEDAW).
Hatua
nyingine ambazo Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania itachukua katika
miaka 15 ijayo ili kuhakikisha usawa wa kijinsia nchini ni zifuatazo:
Kuendeleza na kuunga mkono upatikanaji wa raslimali fedha zinazolenga kuongeza usawa wa kijinsia kwa mujibu wa Ajenda ya Kugharimia Maendeleo ya Addis Ababa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinatolewa pesa za kutekeleza mipango ya kitaifa na ya Serikali za mitaa za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake.Kuhakikisha utekelezaji wa uwakilishi wa uongozi wa asilimia 50-50 kati ya wanawake na wanaume katika nafasi zote za maamuzi kwenye ngazi zote.Kupatikana na kutumiwa kwa data na habari za ukweli katika utunzi wa sera na utoaji maamuzi ya kukomesha ubaguzi wa kijinsia.Kutunga na utekelezaji mfumo wa uwajibikaji na ufuatiliaji wa haki za kijinsia na haki za akinamama zilizokubaliwa kitaifa na kwenye ngazi ya Serikali za mitaa.
Rais
Kikwete pia amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuhusu hatua za kisera na
kisheria ambazo zimechukuliwa na Tanzania katika miaka ya karibuni
kujenga usawa wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Ardhi ya mwaka
1999 na marekebisho yake ya mwaka 2004 ambayo yanawapa akinamama nafasi
na haki ya kupata, kushikilia, kutumia na kumiliki ardhi.
Hatua
nyingine ni kuwapa wanawake nafasi za maamuzi na uongozi katika nyanja
za kisiasa na maisha ya umma. Katika kutekeleza hilo, idadi ya wabunge
wanawake imeongezeka kutoka asilimia 21.5 ya wabunge wote mwaka 2005
hadi kufikia asilimia 34.5 mwaka huu, mawaziri wanawake wameongezeka
kutoka sita mwaka 2005 hadi kufikia 26 mwaka huu na idadi ya majaji
wanawake imeongezeka kutoka wanane mwaka 2005 hadi kufikia 41 mwaka huu.
Rais
Kikwete amesema kuwa hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni
kupunguza vifo vya wanawake wakati uzazi, kutunga Sheria dhidi ya
ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake na watoto; kuanzishwa
kwa uandaaji wa Bajeti inayotilia maanani mahitaji ya wanawake na
kuongeza uwezekaji wa kiuchumi wa akinamama kupitia kuanzishwa kwa Benki
ya Wanawake Tanzania (TWB) yenye kulenga kutoa mikopo ya masharti nafuu
kwa akinamama wafanyao biashara ndogo ndogo na za kati.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
0 comments:
Post a Comment