METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 2, 2015

WANANCHI WAPINGA VIKALI KAULI YA MBUNGE WA IRINGA MJINI YA KUTOKUNYWA MAZIWA YA ASAS

 Moja ya kada wa Chadema akinunua maziwa ya Asas kama alivyonaswa na mpiga picha wetu

Gari za Msafara wa Mgombea urais CHADEMA, Edward Lowassa ukijaza mafuta kuelekea Njombe  siku moja baada ya mbunge wa Iringa mjini kuzuia wafuasi kunywa maziwa na kununua mafuta kwenye kampuni ya Asas Dairlies Ltd


Na WazoHuru Blog

Katika hali ya kusikitisha na kushangaza mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Iringa, Mch Peter Simion Msigwa ametoa matamshi ya kusikitisha kwa kuwazuia wafuasi wa Chadema na wakazi wa Iringa kutonunua maziwa wala kujaza mafuta katika kituo cha mafuta kinachomilikiwa na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani iringa.

Msigwa ambaye amekuwa mbunge wa Jimbo la Iringa mjini Mkoani iringa kwa kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2010 hadi mwaka 2015 ameyasema hayo wakati wa mkutano wake wa ufunguzi wa kampeni Mkoani humo uliofanyika 30/8/2015 kwenye uwanja wa Gangilonga na kuhutubiwa pia na aliyekuwa waziri mkuu ambaye kwa sasa ni mgombea Urais kwa tiketi ya CHADEMA, Edward Lowassa.
 Msigwa ambaye awali katika mkutano huo alitarajiwa kunadi sera na ilani ya CHADEMA ikiwa ni pamoja na kuzungumzia kuhusiana na kauli yake aliyoitoa katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa wakati wa mkutanowa kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa kipindi cha miaka mitano, hali ilikuwa tofauti baada ya wanachi kusikia wakizuiwa kunywa maziwa jambo ambalo limewasikitisha kwa kiasi kikubwa.

Wachambuzi wa maswala ya siasa mjini iringa wameeleza kushangazwa na aina ya kampeni inayofanywa na mchungaji huyo mwaka huu kwa kushindwa kuwaeleza wananchi wake alichokifanya kwa kipindi cha miaka mitano wakati akiwa mbunge na anataraji kufanya nini kwa kipindi kingine anchokiomba kuanzia 2015-2020, badala yake ameingia kwenye aina ya siasa zisizo kuwa na muelekeo wa maendeleo ya mjini Iringa.

Pamoja na maziwa yanayotengenezwa na kampuni ya Asas Dairies Ltd ya mkoani Iringa ambapo kwa mwaka wa tatu mfululizo zimeendelea kushikilia tuzo ya ubora na kuwa kampuni bora kuliko makapuni mengine ya maziwa hapa nchini huku kampuni hiyo ikitoa ajira kwa wananchi wengi lakini bado mbunge huyo ameona si jambo muhimu.

Kampuni ya Asas Dairies Ltd ambayo ni moja kati ya makampuni ya kizalendo nchini na moja kati ya makampuni yaliyopata kupewa tuzo ya ulipaji kodi mzuri na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ilishinda katika maadhimisho ya wiki ya maziwa mwaka huu yaliyofanyika wilayani Babati mkoani Manyara kwa kushindanisha kampuni zaidi ya 20 .

Wachambuzi hao wamesema kuwa ni jambo la ajabu na aibu kwa mbunge huyo ambaye pia ni mchungaji kutumia vibaya majukwaa ya siasa kwa kuchafua biashara za baadhi ya kampuni mjini Iringa ikiwamo kampuni ya Asas Dairies Ltd huku wakihoji kama wanazuiwa kunywa maziwa mbadala wake ni nini.?

Hata hivyo pamoja na matamshi yake hayo bado wafuasi wa CHADEMA wameonekana kuyapuuza baada ya leo moja ya kada wa chadema kukutwa akinunua maziwa hayo wakati akiwa sare ya CHADEMA.

Alipoulizwa ni kwanini amepingana na kiongozi wake ndani ya chama, kijana huyo aliyeombwa jina lake kutotajwa alisema yeye sio mfuasi wa siasa taka zinazofanywa na Msigwa kwani maneno ya mgombea huyo hayawezi kuimarisha afya yake badala yake mwenye uwezo wa kuimarisha ni afya yake ni namna anavyopangilia vyakula vyake ikiwa ni pamoja na kunywa maziwa yanayotengenezwa na kampuni ya Asas Daries Ltd.

Ikumbukwe wazi kwamba siku moja baada ya mkutano huo wa kuzuia wafuasi wa Chadema kununua mafuta kwenye vituo vya mafuta vya Asas bado hali ilikuwa tofauti baada ya msafara wa mgombea urais Kupitia CHADEMA, Edward Lowassa kupanga foleni na kujaza mafuta kwenye kituo mojawapo kilichopo mjini Iringa.

Sambamba na hayo bado inajidhihirisha wazi kwamba siasa za mwaka huu zinalekea kuwa ngumu kwa Mch Msigwa aliyepigiwa kura na wananchi mjini Iringa kwa hasira za kukatwa mgombea waliyempenda ndani ya ccm Fredrick Mwakalebela na kuwekwa aliyekuwa mshindi wa pili kwenye kura za maoni Monica Mbega.

Mwakalebela aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama cha soka TFF nchini, anaonekana kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wafuasi wa CCM na CHADEMA kwa ujumla jambo ambalo linatia wasiwasi mkubwa kwa mbunge aliyemaliza muda wake.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com