Naibu waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Angelina Mabula akioneshwa kigingi cha mpaka kati ya Tanzania na Kenya kilichowekwa wakati wa utawala wa muingereza na Mwenyekiti wa kijiji cha Mahandakini wilaya ya Mkinga Nassoro Mbarouk Nassoro wakati wa ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya.
Naibu waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Angelina mabula akitafuta kigingi cha mpaka kati ya Tanzania na Kenya kwa kuchimba eneo ambalo kigingi hicho kilikuwepo katika kitongoji cha Jasini kijiji cha Mahandakini wilaya ya Mkinga mkoa wa Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro.
Naibu waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Angelina Mabula akiangalia baadhi ya nyumba zilizojengwa katika mpaka wa Tanzania na Kenya katika kijiji cha Mahandakini wilaya ya Mkinga mkoa wa Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya.
Naibu waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Angelina Mabula (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wilaya ya Mkinga mbele ya nyumba iliyojengwa upande ukiwa Tanzania na mwingine Kenya, kuanzia diwani Hassan Bakari Ally (wa nne kulia aliyevaa kofia) kuelekea kulia wako upande wa Kenya.wengine ni Mkuu wa wilaya ya Mkinga Yona Maki (wa pili kulia) na wa tatu kushoto ni mbunge wa jimbo la Mkinga Dustan Kitandula.
Naibu waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Angelina mabula akieleza jambo mara baada ya kupata maelezo juu ya uwekezaji mkubwa wa kiwanda cha Saruji, nishati ya umeme joto, mabegi, vifaa vya ujenzi pamoja na bandari ndogo katika eneo la Mtimbwani wilaya ya Mkinga mkoa wa Tanga kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Mkinga Yona Maki wakati alipofanya ziara ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya.
Na Mwandishi Maalum,
Mkinga Tanga
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amebaini uwepo ya nyumba za
watanzania zilizojengwa katikati ya mpaka wa Tanzania na Kenya huku eneo moja
la nyumba hizo likiwa upande wa Kenya.
Katika ziara yake ya
kukagua mpaka kati ya Tanzania na Kenya eneo la Horohoro mkoa wa Tanga mhe
Mabula alijionea jinsi nyumba zilivyojengwa bila utaratibu wa kuacha umbali wa
mita mia kama eneo huru.
Eneo lililoathirika
zaidi na ujenzi huo, ni katika kitongoji cha Jasini kijiji cha Mahandakini
wilaya ya Mkinga ambapo asilimia kubwa ya wakazi wake wamejenga nyumba zao
zikiwa karibu kabisa na mpaka huku baadhi yake sehemu ikiwa upande wa Tanzania
na nyingine upande wa Kenya.
Hata hivyo, Naibu
Wzairi wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameshuhudia upande wa Tanzania
katika eneo la Horohoro ukiwa umezingatia umbali unaotakiwa kati ya mpaka
ukilinganisha na wakenya wanaoishi kijiji cha Jua kali Lungalunga ambao
wamejenga karibu kabisa na mpaka wa Tanzania.
Kufuatia hali hiyo kuna
uwezekano mkubwa wakazi wanaoishi katika maeneo hayo ya mpakani kukumbwa na
zoezi la kubomolewa nyumba zao ingawa
kwa sasa kuna mazungumzo yanayoendelea baina ya Tanzania na Kenya kuhusu
umbali gani pande hizo zinaweza kukubaliana ili kunusuru baadhi ya wananchi wa
pande zote mbili.
Akizungumza katika
ziara yake ya kukagua mpaka kati ya Tanzania na Kenya, Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amesema, kwa sasa umbali
unaotambulika kama eneo huru baina ya Tanzania na Kenya ni mita mia moja ingawa
kuna mazungumzo yanayoendelea katika ngazi ya wataalamu juu suala la umbali wa
eneo huru.
Kwa mujibu wa Mabula,
pamoja na sheria kuweka bayana kuwa umbali unaotakiwa katika eneo huru kati ya
Tanzania na Kenya ni mita mia moja lakini pande hizo zinaweza kukubaliana kama
ilivyofanyika kwa nchi ya Uganda na Burundi ambapo kwa Uganda eneo huru
litakuwa mita thelathini huku Burundi likiwa mita kumi na mbili na nusu.
Amesema, ukaguzi wa
mipaka anaoufanya una lengo la kuhakikisha mipaka ya Tanzania na nchi jirani
inakuwa katika hali nzuri hasa ikizingatiwa alama za mipaka zilizopo ni za muda
mrefu huku baadhi yake zikiwa zimeharibika.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesisitiza kuwa, kwa sasa Tanzania haina mgogoro
na Kenya juu ya mipaka na kinachofanyika ni kuimarisha usalama wa nchi zote
mbili hasa ikizingatiwa njia za panya ziko nyingi.
Mabula amesema, awamu
ya kwanza ya kuweka alama za mipakani itafanyika katika mipaka baina ya
Tanzania na Kenya pamoja na mpaka kati ya Tanzania na Uganda na fedha yote kwa
ajili ya kazi hiyo imeshatolewa kinachosiriwa ni kuanza tu kwa zoezi.
Mkuu wa wilaya ya
Mkinga Yona Maki alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mabula kuwa Wilaya yake imekuwa lango la raia wanaokimblia afrika kusini, dawa
za kulevya kama mirungi na mpango wa wilaya ni kutaka kufyeka miti na vichaka
vilivyopo katika mpaka kati ya Tanzania na Kenya.
Aidha, amesema wilaya
ya Mkinga ina tatizo la wahamiaji waloweza na zoezi la kuwatambua limeanza ili kuwabaini sambamba na kuthibiti
vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amehitimisha ziara yake ya siku
kumi na mbili mkoa wa Tanga, ziara iliyokuwa na lengo la kukagua mfumo wa
ukusanyaji kodi ya ardhi pamoja na
uhamasishaji ulipaji kodi hiyo ambapo
ziara ilianzia mkoa Mara, Arusha na Kilimanjaro.
-----------------------------Mwisho------------------------------------------------------------------
0 comments:
Post a Comment