METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 3, 2015

WAKONGWE SAFARI KWA LOWASA,,,,


 Mbunge wa Segerea, Dk Makongoro Mahanga Mbunge wa Segerea, Dk Makongoro Mahanga akionyesha karatasi za kura zinazodaiwa kuwa zilikwishapigwa zilizokamatwa wakati wa upigaji wa kura za maoni CCM juzi. Dk Makongoro alitangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kujiunga Chadema kwa kile alichodaia ni uvunjifu wa sheria na hujuma dhidi yake. Picha na Venance Nestory
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga ametangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema baada ya kushindwa katika kura za maoni kwa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Segerea.
Dk Mahanga amechukua uamuzi huo ikiwa ni wiki moja tangu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ahamie katika chama hicho kikuu cha upinzani baada ya kukosa nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM.
Dk Mahanga ambaye amedumu kwenye nafasi ya unaibu waziri kwa kipindi chote cha Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, alisema jana kuwa amejitoa katika chama hicho kwa sababu utaratibu uliotumika katika uchaguzi wa Segerea ulitawaliwa na vitendo vya rushwa na njama zilizofanywa na viongozi wa kitaifa wa CCM ili kuhakikisha anaondolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jana, Dk Mahanga alidai kuwa baadhi ya wagombea katika jimbo hilo walianza kampeni mwaka 2013 jambo ambalo ni kinyume cha sheria za chama.
“Nimetoa malalamiko yangu mara kadhaa kwa uongozi wa CCM wilaya, mkoa na Taifa lakini viongozi hao hawakuchukua hatua yoyote. Hii inaonyesha wazi kuwa nao walikuwa ni sehemu ya mpango huo,” alisema Dk Mahanga.
Alisisitiza kuwa hakubaliani na mchakato uliotumika katika kumpata mshindi kwa sababu viongozi wa kata zote za Jimbo la Segerea walimbeba mgombea mmoja na kuzunguka naye kwenye matawi kinyume cha matakwa ya kanuni za CCM.
Dk Mahanga alisema fedha ziligawiwa kwa muda mrefu na siku ya kupiga kura, baadhi ya maeneo wapigakura walipewa Sh10, 000 na kadi mpya zenye majina feki zilizowawezesha kushiriki.
Alisema operesheni ya kuhakikisha kwamba anaondoka kwenye jimbo hilo ilianza muda mrefu, lakini ilishika kasi zaidi baada ya vikao vya CCM Taifa vya kusaka mgombea urais, mjini Dodoma.
“Familia ya kigogo mmoja wa CCM Taifa iliyokuwa inaishi jirani na mimi kule Dodoma iliamua kuwasakama wanafamilia wangu ikiwaeleza kwamba baada ya Lowassa ni zamu ya baba yao (mimi), lazima niondoke ubunge Segerea kwa gharama yoyote,” alisema.
Alisema hata baada ya hapo, kauli kama hizo ziliendelea wakati wote wa kampeni za ubunge na fedha nyingi ziliingizwa jimboni na kufikia mikononi mwa mmoja wa wagombea ambaye alianza kuzigawa kwa wingi na jeuri.
Dk Makongoro alisema sababu nyingine ya kupigwa vita na CCM ni urafiki wake na Lowassa ambaye tayari amehamia Chadema na kudai kwamba, mara kadhaa aliwahi kuonywa juu ya urafiki wao.
Unaibu waziri
Alisema kigogo mmoja serikalini aliwahi kumwambia kwamba kama ataendelea kuwa karibu na Lowassa hatapanda cheo na ataendelea kuwa naibu waziri siku zote. Alisema ulifika wakati alikata tamaa na kutaka kuacha unaibu waziri lakini alishauriwa asifanye hivyo.
“Mimi ndiye naibu waziri pekee ambaye nimekaa miaka 10. Wamekuja vijana wadogo ambao hawana uzoefu na wakapewa uwaziri, mimi nikiendelea kuwa naibu waziri, inakatisha tamaa sana,” alisema.
Dk Mahanga alisema uhusiano wake na Lowassa ni wa muda mrefu na amekuwa rafiki wa familia. Alisema alipokuwa kijana alikuwa anavutiwa na Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa, lakini baada ya Lowassa kujiuzulu mwaka 2008 walikuwa karibu zaidi.
“Nampenda Lowassa kutokana na utendaji kazi wake, akipewa majukumu ya kiserikali anayatekeleza kikamilifu,” alisema na kusisitiza kuwa uongozi wa juu wa CCM unafinyanga demokrasia na kuwanyima wananchi fursa ya kuchagua viongozi wao.
“Ninatangaza kuanzia leo (jana) ninahamia Chadema na unaibu waziri wangu unakoma kuanzia sasa. Nimeshamwagiza dereva wangu arejeshe gari la Serikali,” alisema mbunge huyo wa Segerea.
Mtatiro amkaribisha Ukawa
Mara baada ya Dk Mahanga kutangaza uamuzi huo, Julius Mtatiro anayewania ubunge katika jimbo la Segerea kupitia CUF, aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook: “Comrade Makongoro Mahanga! Karibu sana Ukawa. Kama unalitaka Jimbo la Segerea njoo tushindanishwe kwa sifa, uwezo na vigezo.
“Natambua utakuwa na mchango mkubwa sana kwa ushindi wa Ukawa lakini lazima uwe tayari kumuunga mkono mgombea wa Ukawa ambaye atapitishwa ikiwa si wewe. Huku Ukawa hakuna kususia, kuna kushirikiana na kupambana tu.”
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com