METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 15, 2015

POLISI MKOANI DODOMA WAFAFANUA KUHUSU MABURUNGUTU YA NOTI.

    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP David Misime

    Napenda kutoa taarifa fupi kuhusu tukio lililotokea tarehe 11/07/2015 majira ya saa 10:00 hrs huko katika Hoteli ya St. Gasper hapa mjini Dodoma, kuwa wananchi walitoa taarifa majira ya saa nne asubuhi kwamba kuna mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia amekamatwa na wananchi akiwa na fedha nyingi na kuna vurugu kubwa.

    Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi Mkoani hapa lilifika eneo la tukio ili kuona kama taarifa hizo ni za kweli.

    Askari walithibitisha kuwa ni kweli walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia ambaye alijulikana kwa jina la AMIT KEVALRAMANI mwenye umri wa miaka 31, Mhindi, Mfanyabiashara, Mkazi wa Dar es Salaam akiwa na fedha kiasi cha Tshs. 722,500,000/= ambacho alipohojiwa alisema kuwa tarehe 10/07/2015 alifika Dodoma kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka.
    Alipofika Dodoma tarehe 10/07/2015 majira ya asubuhi alifikia katika Hoteli ya St. Gasper na tarehe 11/07/2015 aliamua kurudisha fedha benki kutokana na kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka na wenye viashiria vya vurugu.
    Akiwa katika harakati ya kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa katika eneo la Hoteli ya St. GASPER walimtilia mashaka na kumzuia asiondoke na ndipo taarifa zilitolewa polisi. Mashaka ya watu hao yalitokana na vuguvugu za kisiasa/mchakato wa uchaguzi kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu wanahonga wajumbe. Taarifa za aina hiyo ambazo hata Jeshi la Polisi lilikuwa limepokea bila uthibitisho.
    Katika tukio hili na uchunguzi tulioufanya tumebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwa kuwa hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo.
    Aidha imethibitika fedha hizo ni mali yake halali na kwa kuwa hakuna ushahidi mwingine uliyo thibitisha vinginevyo amerejeshewa fedha zake
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com