Mbinu za kiufundi za klabu ya Yanga zilizoipa
ubingwa wa Ligi Kuu, sasa zimehamishiwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa,
‘Taifa Stars’ inayojiandaa kuikabili Uganda Cranes, Jumamosi.
Kocha Hans Pluijm juzi aliibukia kwenye
mazoezi ya Stars yaliyofanyika Boko, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na
kushirikiana na msaidizi wake, Boniface Mkwasa.
Stars inayoondoka leo kwenda Kampala,
Uganda mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika
kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan 2016) ilikuwa ikijinoa chini ya
Mkwasa. Katika mchezo wa awali, Stars ilibugizwa mabao 3-0 wiki moja iliyopita.
Katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja
wa Boko Veteran, Pluijm alionekana akitoa ushauri wa kiufundi kwa benchi la
ufundi la Stars linaloongozwa na Mkwasa, ambaye ni msaidizi wake ndani ya
Yanga.
Pluijm aliyeongozana na meneja wa klabu yake,
Hafidh Saleh mara nyingi alionekana akimpa maelekezo mshauri wa ufundi wa
Stars, Abdallah Kibaden aliyekuwa akimfikishia moja kwa moja Mkwasa.
Muda huo Mkwasa alikuwa akiendelea na kazi ya
kuwanoa mabeki na viungo wakabaji wa Stars, huku kocha msaidizi, Hemed Morocco
akiwapa makali washambuliaji.
Akizungumza na gazeti hili baada ya mazoezi hayo,
Pluijm alisema yeye akiwa kocha anayefanya kazi yake nchini haoni tatizo lolote
kutoa ushauri wa kitaalamu unaoweza kuisaidia timu ya Taifa.
“Nimekuja hapa kutazama mazoezi na ninapoona kuna
jambo la kusaidia kiufundi sioni shida kusaidiana na benchi la ufundi kwa
sababu hii ni timu ya Taifa ambayo inatakiwa iungwe mkono na wananchi wote,”
alisema Pluijm.
Hata hivyo, Pluijm alisifu mabadiliko yaliyopo
sasa kwenye timu ya Taifa na kusema kuwa yatarudisha imani ya mashabiki wa soka
nchini huku akitaka benchi la ufundi liungwe mkono na kupewa muda zaidi.
“Tatizo kubwa kwa timu hii lilikuwa ni wachezaji
kushindwa kujua wajibu wao jambo ambalo hivi sasa halipo tena. Kuna makosa
mengi yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza, hasa kuwaachia Uganda eneo kubwa
la uwanja hali iliyowafanya wawe na uhuru mkubwa wa kucheza.
“Naamini kwenye mechi ijayo hilo halitojitokeza
tena ingawa sidhani kama tunaweza kufunga mabao nne kwao,” aliongeza Pluijm.
Hata hivyo, Mkwasa amekuwa akionekana Yanga
kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye Uwanja wa Karume, Dar es
Salaam nyakati za asubuhi, hivyo kuwashangaza mashabiki wengi kuwa
anawezaje kuzitumikia timu mbili kwa wakati mmoja.
0 comments:
Post a Comment