Friday, July 3, 2015

MBINU: Yanga yaivamia Stars



 
Mbinu za kiufundi za klabu ya Yanga zilizoipa ubingwa wa Ligi Kuu,  sasa zimehamishiwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ inayojiandaa kuikabili Uganda Cranes, Jumamosi.
Kocha Hans Pluijm juzi  aliibukia kwenye mazoezi ya Stars yaliyofanyika Boko, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kushirikiana na msaidizi wake, Boniface Mkwasa.
Stars inayoondoka leo kwenda  Kampala, Uganda mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan 2016) ilikuwa ikijinoa chini ya Mkwasa. Katika mchezo wa awali, Stars ilibugizwa mabao 3-0 wiki moja iliyopita.
Katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veteran, Pluijm alionekana akitoa ushauri wa kiufundi kwa benchi la ufundi la Stars linaloongozwa na Mkwasa, ambaye ni msaidizi wake ndani ya Yanga.
Pluijm aliyeongozana na meneja wa klabu yake, Hafidh Saleh mara nyingi alionekana  akimpa maelekezo mshauri wa ufundi wa Stars, Abdallah Kibaden aliyekuwa akimfikishia moja kwa moja Mkwasa.
Muda huo Mkwasa alikuwa akiendelea na kazi ya kuwanoa mabeki na viungo wakabaji wa Stars, huku kocha msaidizi, Hemed Morocco akiwapa makali  washambuliaji.
Akizungumza na gazeti hili baada ya mazoezi hayo, Pluijm alisema yeye akiwa kocha anayefanya kazi yake nchini haoni tatizo lolote kutoa ushauri wa kitaalamu unaoweza kuisaidia timu ya Taifa.
“Nimekuja hapa kutazama mazoezi na ninapoona kuna jambo la kusaidia kiufundi sioni shida kusaidiana na benchi la ufundi kwa sababu hii ni timu ya Taifa ambayo inatakiwa iungwe mkono na wananchi wote,” alisema Pluijm.
Hata hivyo, Pluijm alisifu mabadiliko yaliyopo sasa kwenye timu ya Taifa na kusema kuwa yatarudisha imani ya mashabiki wa soka nchini huku akitaka benchi la ufundi liungwe mkono na kupewa muda zaidi.
“Tatizo kubwa kwa timu hii lilikuwa ni wachezaji kushindwa kujua wajibu wao jambo ambalo hivi sasa halipo tena. Kuna makosa mengi yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza, hasa kuwaachia Uganda eneo kubwa la uwanja hali iliyowafanya wawe na uhuru mkubwa wa kucheza.
“Naamini kwenye mechi ijayo hilo halitojitokeza tena ingawa sidhani kama tunaweza kufunga mabao nne kwao,” aliongeza Pluijm.
Hata hivyo, Mkwasa amekuwa akionekana Yanga kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye Uwanja wa Karume,  Dar es Salaam nyakati za asubuhi, hivyo kuwashangaza  mashabiki wengi kuwa anawezaje kuzitumikia timu mbili kwa wakati mmoja.

No comments:

Post a Comment