ASKARI
wanne na raia watatu wameuawa baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi
kuvamia Kituo cha Polisi cha Sitakishari kilichopo Ukonga katika
Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam.
Tukio
hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana baada ya majambazi kufika kituoni
hapo saa tano usiku kama wananchi wanaohitaji huduma kituoni hapo,
lakini baada ya kuhojiwa na askari waliokuwa zamu waliwafyatulia risasi
askari hao na kuwaua wanne.
Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu, akithibitisha alisema miongoni
mwa raia waliouawa ni mmoja wa waliofika kituoni hapo akiwa ameongozana
na majambazi waliotekeleza tukio hilo la kutisha.
“Inasemekana
kundi hili la majambazi lilifika kama wananchi wanaohitaji huduma,
lakini walipoonekana tofauti na raia wema wakaulizwa nini wanahitaji
kusaidiwa, ndipo waliwafyatulia risasi na kuwaua askari waliokuwepo hapo
na kuendelea kuelekea ndani ya kituo,” alisema Mangu.
Alisema
katika 'fyatua fyatua’ hiyo ya risasi, majambazi hao waliwaua askari
wanne papo hapo na raia watatu. IGP Mangu alisema baada ya kufanya
mauaji hayo katika tukio linalotajwa kudumu kwa takribani dakika 45,
kabla ya kuzimwa na polisi, majambazi hao walipora silaha ambazo
zilikuwepo kituoni hapo na idadi yake haijajulikana hadi hapo utafiti
utakapokamilika.
“Uharibifu
mkubwa umetokea ikiwemo wizi wa silaha ambazo hadi hivi sasa idadi yake
haijajulikana hadi utafiti ukamilike,’’ alisema. Kwa upande wa
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam
ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadick alisema wananchi wasiwe na
hofu kwani usalama wao unalindwa na kikubwa watoe ushirikiano kwa polisi
ili kuweza kuwabaini wahalifu hao.
“Tukio
hili ni la kusikitisha sana ambalo limepoteza uhai wa askari wetu pamoja
na wananchi. Kila mtu anapaswa kulikemea na kutoa ushirikiano ili
tuweze kuwabaini hawa waliotenda tukio hili kwani nina imani wanaishi
ndani ya jamii yetu na tunawafahamu,” alisema Sadick.
Alisema
wahalifu hawa wanatumia usafiri ambao unajulikana kwa wananchi, wanaishi
na kufanya mambo mengi ndani ya jamii; hivyo wananchi wasiache kutoa
taarifa mahali walipo ili kufanikisha kukamatwa kwao na kufikishwa
kwenye vyombo vya sheria.
Kwa
mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema saa tano usiku walisikia
milio ya risasi kituoni hapo na kudhani kuwa watuhumiwa wametoroka na
kwamba polisi wanafanya juhudi za kuwarudisha, lakini hali ikawa sio
shwari baada ya milio ya risasi kuongezeka.
“Tulikuwa
tumekaa hapa nje, mara tukasikia mlio wa risasi kisha ikaendelea kwa
kasi, tukakimbilia ndani na kujifungia maana tukio la milio ya risasi
lilichukua muda mrefu sana kama saa moja hivi,” alisema mmoja wa
mashuhuda aliyepo jirani na kituo hicho ambaye hakupenda jina lake
liandikwe.
Kutokea
kwa tukio hili la uvamizi katika kituo cha polisi ni mwendelezo wa
uvamizi ambao umekuwa ukitokea mara kwa mara vituo vya polisi kuvamiwa
na watu wenye lengo la kupora silaha na kuwaua askari wanaowakuta ndani
ya vituo hivyo
0 comments:
Post a Comment