RAIS wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema uteuzi wa mgombea wa CCM katika
nafasi ya rais wa Jamhuri ya Muungano katika uchaguzi mkuu, Dk John
Magufuli ndio chaguo sahihi la kupambana na upinzani na kuleta ushindi
katika CCM na kushika dola.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili Zanzibar kutoka Dodoma,
Dk Shein alimtaja Magufuli kama kiongozi hodari muaminifu mwenye shauku
kubwa ya kuleta maendeleo ya nchi yake.
Dk Shein
katika mkutano mkuu uliomalizika Dodoma hivi karibuni Halmashauri Kuu ya
Chama Cha Mapinduzi imemwidhinisha kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya CCM tayari kupambana na chama kikuu cha CUF.
Alisema,
Magufuli katika nyadhifa mbalimbali alizoshika ameonesha uhodari wa
kuchapa kazi na uzalendo pamoja na kusimamia majukumu yake pamoja na
walio chini yake. Alifahamisha kwamba ndiyo kigezo sahihi cha kupambana
na wapinzani na kuleta maendeleo ya wananchi wa Tanzania.
‘’Mimi
namfahamu vizuri sana Magufuli nimefanya kazi naye katika kipindi cha
miaka 9 katika baraza la mawaziri nikiwa makamu wa rais......ni mchapa
kazi hodari, mwadilifu mwenye mapenzi makubwa na wananchi
wake,’’alisema.
Kwa mfano
alisema katika Wizara zote alizopata kufanya kazi alionesha uwezo wa
ubunifu wa kuleta maendeleo akizitaja Wizara ya Uvuvi pamoja na Ujenzi.
Aidha
alimpongeza kwa kumteua Samia Suluhun Hassan, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais kuwa mgombea mwenza huku Chama Cha Mapinduzi kikiweka
rekodi ya kuwa na mgombea mwenza mwanamke.
Alisema
Samia ameonesha uwezo wa kazi katika nafasi mbalimbali alizopata
kuzishika tangu akiwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi
Muungano.
Alifahamisha
kwamba Demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi imeimarika kwa kiwango
kikubwa ambapo nafasi za wanachama mbalimbali kugombea nafasi za juu za
uongozi ni kubwa sana ikiwemo wanawake.
Kwa
mfano, alisema Chama Cha Mapinduzi kimeweka historia kubwa ya kuteua
wanawake wawili kuingia katika hatua ya mwisho ya uteuzi wa tatu bora.
‘’Hicho ndicho Chama Cha Mapinduzi demokrasia yake katika makundi
mbalimbali imekuwa kwa kiwango kikubwa ikiwemo wanawake kushirikishwa
katika mchakato wa hatua za mwisho na kushika nafasi ya mgombea
mwenza,’’ alisema.
Alipoulizwa
kuhusu wingi wa wagombea wa nafasi ya juu ya urais, alisema demokrasia
katika Chama Cha Mapinduzi imepanuka kwa kiwango kikubwa tofauti na
vyama vyengine vya siasa.
Alisema
katika mchakato wa nafasi ya urais jumla ya wanachama wa CCM 42
walijitokeza kuwania nafasi hiyo tofauti na miaka ya 2000 ambapo
walijitokeza wanachama 17. ‘’Chama Cha Mapinduzi kinajengwa kwa nguvu ya
msingi mmoja mkubwa ambao ni demokrasia iliyopevuka inayotoa makundi
mbalimbali ya wanachama kuwania nafasi za juu za uongozi,’’alisema.
Akisoma
risala ya wananchi wa mikoa sita kichama, naibu katibu mkuu wa Umoja wa
Vijana (UVCCM Zanzibar), Shaka Hamdu alisema wamefurahishwa na maamuzi
ya vikao vya chama kuwateuwa wagombea wa nafasi za juu za urais kwa
upande wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
Shaka
alisema wanachama wa CCM Zanzibar wanaunga mkono uteuzi huo wa majina ya
viongozi hao ambao watapeperusha bendera ya chama kuelekea uchaguzi
mkuu wa mwaka huu na kukileta ushindi chama.
‘’Wanachama
wa mikoa sita matumaini yao makubwa kwamba wagombea wa nafasi za urais
kuanzia John Magufuli nafasi ya urais wa Muungano pamoja na Dk Ali
Mohamed Shein kwa nafasi ya urais wa Zanzibar kwamba ni uteuzi sahihi wa
wagombea wenye sifa watakaokiletea chama ushindi,’’alisema.
Mamia ya
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla wamejitokeza
katika mapokezi ya mgombea wa urais wa Zanzibar kuanzia uwanja wa ndege
wa Abeid Amaan Karume hadi katika makao makuu ya CCM Kisiwandui.
0 comments:
Post a Comment